1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Upigaji kura waendelea kwa amani katika uchaguzi mkuu Nepal

5 Machi 2026

Upigaji kura umefanyika kwa amani katika uchaguzi wa kwanza wa kitaifa nchini Nepal tangu maandamano yenye vurugu yaliyoongozwa na vijana kuilazimisha serikali kuondoka madarakani mnamo Septemba.

https://p.dw.com/p/59pfP
Kampeni na upigaji kura hadi Alhamisi hazijavurugwa na matukio yoyote ya ghasia, maafisa walisema.
Kuna wapiga kura wapatao milioni 19 waliojiandikisha miongoni mwa watu karibu milioni 30 nchini humo.Picha: Prakash Mathema/AFP

Vikosi vya usalama viliweka doria mitaani na vituo vya kupigia kura kote katika taifa hilo la Milima ya Himalaya lenye watu wapatao milioni 30 huku wapiga kura wakipanga foleni kupiga kura zao. Shughuli ya kuhesabu kura inatarajiwa kuanza baadaye Alhamisi, huku matokeo yakitarajiwa mwishoni mwa wiki. Kampeni na upigaji kura hadi Alhamisi hazijavurugwa na matukio yoyote ya ghasia, maafisa walisema.

"Kuna msisimko mkubwa kuhusu uchaguzi huu miongoni mwa watu, na tunatarajia idadi ya wapiga kura kuwa angalau 65%," kaimu kamishna mkuu wa uchaguzi wa Nepal Ram Prasad Bhandari alisema.

Mamlaka zililipiga marufuku magari kuingia mitaani na kukataza mikutano ya kisiasa na mikusanyiko ya umma. Aina zote za kampeni zimepigwa marufuku siku ya uchaguzi.

Watu walijaa katika vituo vya kupigia kura kuanzia milimani kaskazini hadi wilaya za tambarare za kusini. Katika uwanja mkuu wa mji mkuu wa Kathmandu, wanaume na wanawake walisimama katika mistari tofauti huku maafisa wa polisi na wanajeshi wakidumisha ulinzi mkali kuzunguka eneo hilo.

Vikosi vya usalama vimeweka doria mitaani
Mamlaka zililipiga marufuku magari kuingia mitaani na kukataza mikutano ya kisiasa na mikusanyiko ya umma.Picha: Prakash Mathema/AFP

"Nilikuja kupiga kura hasa kwa sababu ya maandamano na watu wengi walitoa maisha yao kwa matumaini ya mabadiliko, kwa matumaini ya kuona Nepal bora," alisema Luniva, mpiga kura wa mara ya kwanza. "Natumaini, nataka kuona nchi yangu ikiimarika kutokana na damu yote iliyomwagika."

Wengine walikuwa na matumaini kama hayo kwamba uchaguzi huo utaweza kuleta mabadiliko chanya kwa taifa hilo la Himalaya baada ya miezi kadhaa ya machafuko ya kisiasa.

Kulingana na Tume ya Uchaguzi ya Nepal, kuna wapiga kura wapatao milioni 19 waliojiandikisha miongoni mwa watu karibu milioni 30 nchini humo.

Mamilioni ya Wanepali wanaoishi ng'ambo hawawezi kushiriki katika upigaji kura. Inakadiriwa kuwa raia milioni 3 wanafanya kazi nje ya nchi — kwa kiasi kikubwa katika Mashariki ya Kati, Asia ya Kusini-mashariki na India jirani — na hawawezi kupiga kura kwa sababu nchi hiyo bado haina mfumo unaoruhusu upigaji kura kutoka nje ya nchi.

Wapiga kura wanawachagua moja kwa moja wajumbe 165 katika Baraza la Wawakilishi. Viti 110 vilivyobaki katika baraza hilo lenye wanachama 275 vitagawanywa kupitia mfumo wa uwakilishi sawia, ambapo vyama vya siasa huteua wabunge kulingana na idadi yao ya kura.

Waandamanaji wanapiga kelele na kuchoma matairi huku wakizuia Mtaa Mkuu huko Birgunj
Maandamano ya kupinga ufisadi na utawala mbovu yalichochewa na marufuku ya mitandao ya kijamiiPicha: Jiyalal Saah/AP Photo/picture alliance

Uchaguzi huo unaonekana sana kama ushindani wa pande tatu, uliochochewa na kukatishwa tamaa kwa wapiga kura kutokana na ufisadi ulioenea na wito wa kutaka uwajibikaji mkubwa wa serikali.

Chama National Independent, kilichoanzishwa mwaka wa 2022, kinachukuliwa kuwa na nafasi kubwa ya kushinda, kikitoa changamoto kubwa kwa vyama viwili vilivyotawala kwa muda mrefu: Nepali Congress na Chama cha Kikomunisti cha Nepal (Unified Marxist-Leninist).

Mgombea wa uwaziri mkuu wa chama kipya ni mwanamuziki wa mtindo wa kufoka aliyegeuka kuwa mwanasiasa Balendra Shah, ambaye alishinda kinyang'anyiro cha umeya wa Kathmandu mwaka wa 2022 na kuibuka kama mtu aliyokuwa mstari wa mbele katika vuguvugu la maandamano ya umma 2025 yaliyomwondoa madarakani Waziri Mkuu wa zamani Khadga Prasad Oli.

Shah, mwenye umri wa miaka 35, ameitumia hasira ya umma dhidi ya vyama vya siasa vya kitamaduni. Alisisitiza afya na elimu kwa Wanepali maskini kama kipaumbele muhimu wakati wa kampeni yake.

Maandamano ya kupinga ufisadi na utawala mbovu yalichochewa na marufuku ya mitandao ya kijamii kabla ya kugeuka kuwa vuguvugu la mapinduzi dhidi ya serikali. Watu kadhaa waliuawa na mamia kujeruhiwa wakati waandamanaji waliposhambulia majengo ya serikali na polisi kuwafyatulia risasi.