1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yasema takriban watu 100 walitekwa ama kupotezwa Syria

7 Novemba 2025

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema leo kuwa takriban watu 100 wamerekodiwa kutekwa nyara ama kutoweka nchini Syria tangu mwanzoni mwa mwaka huku kukiwa na ripoti mpya za watu kuendelea kupotezwa.

https://p.dw.com/p/53HIu
Syria Latakia 2025 | vikosi vya serikali
Maafisa wa jeshi la serikali ya Syria wakielekea Latakia kupambana na wapiganaji wanaohusishwa na kiongozi aliyeondolewa madarakani Bashar al-Assad Machi 7, 2025Picha: Moawia Atrash/dpa/picture alliance

Msemaji wa ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa Thameen Al-Keetan, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwamba miezi kumi na moja tangu kuanguka kwa serikali ya zamani nchini Syria, wanaendelea kupokea ripoti zinazotia wasiwasi kuhusu watu kutekwa nyara na kupotezwa kwa nguvu.

Ofisi hiyo imerekodi angalau watu 97 ambao wametekwa nyara au kutoweka tangu Januari mwaka huu, na kusema ni vigumu kupata takwimu sahihi.

Hali ya usalama Syria yafanya kuwe vigumu kuwatafuta watu waliopotea

Pia imesema hali tete ya usalama nchini Syria, kufuatia kuzuka kwa ghasia katika eneo la pwani na mji wa kusini wa Sweida, imefanya kuwa vigumu kuwapata ama kuwafuatilia watu waliopotea kwasababu baadhi wanaogopa kutoa maelezo.

Al-Keetan ameongeza kuwa baadhi ya watu walikabiliwa na vitisho kwa kuzungumza na Umoja wa Mataifa.