UN yapendekeza jeshi kuingilia kati kaskazini mwa Mali | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.11.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

UN yapendekeza jeshi kuingilia kati kaskazini mwa Mali

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon amependekeza kwamba Baraza la Usalama la umoja huo liidhinishe kikosi cha kijeshi cha Umoja wa Afrika kitakachopelekwa kupambana na waasi kaskazini mwa Mali.

Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-moon

Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-moon

Katika taarifa yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon amesema operesheni yoyote kaskazini mwa Mali inaziweka haki za kibinaadamu katika hali ya hatari, lakini kuna umuhimu wa nchi hiyo kuingiliwa kijeshi kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za kibinaadamu na unyanyasaji unaofanywa na wapiganaji wa kigaidi. Amesema Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linataka kuwepo kwa mipango madhubuti ya kijeshi kutoka kwa mataifa ya Afrika kuhusu operesheni hiyo na kuongeza kuwa Umoja wa Mataifa haukuweza kutoa fedha kwa ajili ya shughuli hiyo.

Katika ripoti yake iliyosubiriwa kwa shauku kubwa, Ban amebainisha kuwa suala la jeshi kuingilia kati kaskazini mwa Mali linaweza kuifanya hali tete iliyopo sasa kuwa mbaya zaidi na pia kusababisha ukiukwaji mkubwa zaidi wa haki za binaadamu. Hata hivyo amesema swali la msingi kuhusu jinsi gani kikosi hicho kitaongozwa, kitakuwa endelevu, kitapata mafunzo, vifaa na fedha, bado linabaki bila jibu.

Baadhi ya viongozi wa ECOWAS

Baadhi ya viongozi wa ECOWAS

Amefafanua kuwa iwapo operesheni hiyo itakubalika kimataifa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litatoa muda wa mwaka mmoja wa kupelekwa wanajeshi 3,300 kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi-ECOWAS na Umoja wa Afrika.

Kikosi hicho kitasaidia kuleta utulivu Mali

Amesema kikosi hicho kitaisadia serikali ya Mali kulitwaa tena eneo la kaskazini mwa nchi hiyo kwa lengo la kuleta umoja, amani na uadilifu wa nchi hiyo na kupunguza vitisho vinavyotokana na makundi ya kigaidi na uhalifu unaofanywa kuvuka mipaka. Kikosi hicho kitajulikana kama Kikosi cha Kimataifa kinachoongozwa na Afrika kwa ajili ya Mali-AFISMA. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajia kuujadili mzozo wa Mali Disemba 5, mwaka huu na wanadiplomasia wanasema azimio hilo linaweza likaidhinishwa mwishoni mwa mwaka huu.

Waasi wa kaskazini mwa Mali

Waasi wa kaskazini mwa Mali

Hata hivyo, waratibu wa kijeshi wa Afrika wameuambia Umoja wa Mataifa kuwa operesheni hizo za kijeshi nchini Mali huenda isianze kabla ya mwezi Septemba mwaka ujao kwa sababu kikosi hicho kinahitaji muda wa kutosha kujiandaa na kutokana na msimu wa mvua unaoanza katikati ya mwezi Juni hadi Agosti. Aidha, kwa upande mwingine Umoja wa Ulaya unapanga kupeleka wanajeshi wake 200 nchini Mali kwa ajili ya kusaidia kutoa mafunzo.

Waasi wa Tuareg na wanamgambo wenye itikadi kali za Kiislamu wanaohusishwa na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda, walilidhibiti eneo la kaskazini mwa Mali mwezi Machi mwaka huu baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani kiongozi wa nchi hiyo, Amadou Toumani Toure na hivyo kuweka pengo la uongozi lililosababisha waasi hao kulitwaa eneo hilo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,AFPE
Mhariri: Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com