UN yaadhimisha miaka 70 ya ulinzi wa amani duniani
29 Mei 2018Ni nafasi ya kukumbuka mchango wa wanajeshi wa Umoja wa Mataifa na raia watumishi wa taasisi hiyo zaidi ya 3,700 waliopoteza maisha yao wakiitumikia bendera ya Umoja wa Mataifa tokea 1948, wakiwemo 129 waliouwawa mwaka jana 2017.
Siku hii inasherehekewa wakati Umoja wa Mataifa ukiwa ni chombo cha pekee cha kuendeleza na kuzisaidia nchi zilizoharibiwa kutokana na migogoro na badala yake kuweka mazingira ya kuleta amani ya kudumu katika nchi hizo.
Shughuli za kwanza za kulinda amani zilianzishwa Mei 29 1948, pale Baraza la Usalama lilipoamuru kutumwa kikos kidogo cha wangalizi wa kijeshi wa Umoja wa Mataifa katika Mashariki ya Kati, kuunda kile kilichojulikana kama Kikundi cha kusimamia usitishaji mapigano (UNTSO) kufuatia makubaliano ya kusitisha matumizi ya silaha yaliofikiwa baina ya Israel na mataifa jirani ya Kiarabu.
Kwa zaidi ya miongo saba, zaidi ya watu milioni moja wanaume na wanawake wamekuwa wakitumika chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa katika shughuli 71 za kulinda amani, huku moja kwa moja wakihusika katika kuwahudumia mamilioni ya watu na kulinda maisha yao.
Huduma ya kujitoa mhanga
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanajitolea muhanga na mara nyingi katika maeneo ya hatari na katika mazingira magumu. Muhanga huu pia ni wa familia za wale wanaotoa huduma hizo pamoja na serikali zao.
Kuanzia Sierra Leone hadi jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo , Cambodia, Namibia, El Salvador na kwengineko, askari wa kulinda amani wamesaidia nchi husika kuweza kujitoa kutoka kwenye vita na kuwa na amani.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Liberia (UNMIL) ulifanikiwa kumaliza shughuli zake mwezi Machi mwaka huu, ukiwa ni ujumbe wa 57 wa shughuli za kusimamia amani za Umoja wa Mataifa kufanya hivyo.
Leo hii Umoja wa Mataifa una zaidi ya wanajeshi 100,000, polis na watumishi wa kiraia katika jumbe 14 za kulinda amani katika mabara manne.
Ushirikiano katika kulinda amani
Kwa wakati huu mataifa 124 wanachama yamechangia wanajeshi na polisi pamoja na vifaa muhimu katika harakati za kulinda amani.
Harakati za kusimamia amani ni ushirikiano wa kimataifa na idadi hiyo inaashiria kujizatiti na kujitoa kwa wanacahama wake katika lengo hilo.
Wakati siku ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa ni Mei 29, Umoja wa Mataifa utasherehekea siku hii mwaka huu hapo Juni mosi kwenye makao yake makuu mjini New York .
Sambamba na hayo Umoja huo utakabidhi Medali ya Dag Hammarskjöld kwa walinda amani waliokufa mwaka 2017 wakiwa katika jukumu na utumishi wao wa kusimamia amani.
Barani Afrika mbali ni pamoja na jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ukiwa ujumbe mkubwa kabisa duniani na pia jamhuri ya Afrika Kati.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman
Mhariri: Iddi Ssessanga