1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Itachukua muda mrefu kuidhibiti Ebola

12 Desemba 2014

Mkuu wa masuala ya kupambana na Ebola wa Umoja wa Mataifa Daktari David Nabarro amesema itachukua miezi kadhaa zaidi kabla ya janga la Ebola kuweza kudhibitiwa katika nchi za magharibi mwa Afrika zilizoathirika.

https://p.dw.com/p/1E32c
Picha: picture-alliance/AP Photo/Julien Gregorio, Geneva University Hospital

Daktari Nabarro amesema kuna mabadiliko makubwa ya hali ilivyo katika nchi zilizoathiriwa na Ebola magharibi mwa Afrika katika kipindi cha miezi minne iliyopita kutokana na jinsi serikali husika zinavyoushughulikia ugonjwa huo,hatua zinazochukuliwa na jamii na mchango wa jumuiya ya Kimataifa katika kupamabana nao.

Lakini amesema juhudi zaidi zinahitajika kuudhibiti ugonjwa huo magharibi mwa Sierra Leone na kaskazini mwa Mali ili kupunguza idadi ya visa vipya Liberia na kupunguza maambukizi Mali.

Shirika la afya duniani WHO limekiri kuwa halikuweza kufikia lengo la kuwatenga wagonjwa wote wa Ebola na kuwazika salama waliokufa katika taifa la Sierra Leone kwa asilimia 70 ilipofika tarehe mosi mwezi huu kama ilivyokuwa imetarajia.

Ni vigumu kusawazisha takwimu

WHO imesema inakuwa vigumu kwao kusawazisha takwimu kuhusu visa vya Ebola kwa sababu haijui hasa ni wagonjwa wangapi waliogua Ebola na kuwafuatilia walio karibu nao inakuwa kibarua kigumu.

Mkuu wa masuala ya kupambana na Ebola David Nabarro
Mkuu wa masuala ya kupambana na Ebola David NabarroPicha: imago/Xinhua

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon mwezi uliopita alisema janga hilo la Ebola huenda likadhibitiwa baadaye mwaka ujao.Kiasi ya watu 18,100 wameathirika na 6,500 kati yao wamefariki nchini Guinea,Liberia na Sierra Leone.

Akizungumza na wanahabari hapo jana,Nabarro amsema idadi ya maambukizi mapya yanapungua Liberia na Guinea lakini ugonjwa huo unaendelea kusambaa kwa kasi nchini Sierra Leone.

Rais wa Sierra Leone Ernest Bai Koroma amewataka viongozi wa kimila nchini humo kusitisha mila na desturi kama kugusa miili ya maiti wakati wa mazishi ili kupunguza kusambaa kwa ugonjwa huo.

Koroma amesema anatumai kusitisha maambukizi katika kipindi cha siku ishirini na moja zijazo lakini lengo hilo linaonekana kuwa gumu kufikiwa ikizingatiwa nchi hiyo inarekodi visa kati ya 400 na 500 kila wiki.

Mkuu mpya wa kupambana na Ebola ateuliwa

Huku hayo yakijri,Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon hapo jana alitangaza Ismail Ould Cheikh Ahmed atakuwa mkuu mpya wa operesheni za kupambana na Ebola magharibi mwa Afrika wadhifa uliokuwa ukishikiliwa na Anthony Banbury.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki MoonPicha: picture-alliance/dpa/K. Elfiqi

Ahmed ambaye hivi sasa ni naibu wa mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Libya atafanya kazi kwa karibu na Nabarro na serikali za kanda hiyo ya magharibi mwa Afrika kuanzia mwezi Januari atakapochukua rasmi wadhifa huo.

Wakati huo huo,wizara ya afya ya Mali imetangaza kuwa hakuna kisa kinachosalia cha Ebola nchini humo baada ya mgonjwa wa mwisho kupona na kuruhusiwa kuondoka hospitalini.

Watu sita wamekufa kutokana na Ebola Mali huku wengine wawili wakipona.Hata hivyo WHO haijatangaza rasmi Mali kuwa nchi isio na Ebola, taifa la sita la magharibi mwa Afrika kugundulika kuwa na ugonjwa huo.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/ap

Mhariri: Gakuba Daniel