Umoja wa Mataifa wazuru Ukanda wa Ziwa Chad | Matukio ya Afrika | DW | 02.03.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Umoja wa Mataifa wazuru Ukanda wa Ziwa Chad

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linazuru ukanda wa Ziwa Chad, ambako kwa kiasi kikubwa kunakabiliwa na majanga ya njaa, uasi wa kundi la wapiganaji wa Boko Haram, mabadiliko ya tabia nchi na utawala mbovu

Majanga hayo kwa pamoja yanafanya eneo hilo kuwa moja ya maeneo yanayokabiliwa na mgogoro mkubwa zaidi wa kibinaadamu uliowahi kutokea duniani. 

Wanadiplomasia 15 kutoka chombo hicho cha juu zaidi cha maamuzi ndani ya Umoja wa Mataifa wanatarajiwa kuifanya dunia kutafuta hatua za dharura za kuwanusuru kiasi ya watu Milioni 21 waliopo kwenye nchi nne za Ukanda huo, za Nigeria, Chad, Cameroun na Niger.  

Ziara hiyo huenda pia ikatoa fursa kwa baraza hilo la usalama kuchukua hatua madhubuti zaidi katika kuushughulikia mgogoro ambao kwa kiasi kikubwa umepuuzwa na kushushwa kabisa katika ajenda ya kidiplomasia wakati vita nchini Syria na sudan Kusini vikipamba moto.

Balozi wa Uingereza, Matthew Rycroft amesema, ziara hiyo itaondoa doa kuhusiana na namna taasisi hiyo ya kimataifa inavyokabiliana na majanga ya kibinaadamu, wakati ambapo mwito ukitolewa kwa wafadhili kuja na mipango mipya ya kuzisaidia kifedha nchi za ukanda huo.

Wakiongozwa na Uingereza Ufaransa na Senegal, wajumbe wa  baraza hilo watakutana na viongozi, kufanya mazungumzo na asasi za kiraia na kutembelea makambi nchini Cameroun na Kaskazini Mashariki mwa Nigeria yanayohifadhi kiasi ya watu Milioni 2.3 waliokimbia makazi yao katika ukanda huo.

Mapema wiki iliyopita, kwenye mkutano uliowakutanisha wafadhili wa kimataifa mjini Oslo, Norway, Mkuu wa masuala ya misaada ya kibinaadamu katika Umoja wa Mataifa, Stephen O'Brien alisema nchini 14 zimeahidi kiasi cha Dola Milioni 672 za msaada kwa kipindi cha miaka mitatu ili kukabiliana na njaa katika ukanda huo wa Ziwa Chad iliyosababishwa na ukame, umasikini uliokithiri na kitisho cha Boko Haram.

NIGERIA Hunger und Mangelernährung (Getty Images/AFP/F. Plaucheur)

Raia nchini Nigeria wanatishiwa na njaa kutokana na ukame, Boko Haram na umasikini uliokithiri

 

Kwenye mkutano huo waziri wa mambo ya nje wa Nigeria, Geoffrey Onyeama alisema, watu Milioni 26 wanakabiliwa na uasi wa kundi la Boko Haram, wakati mpango wa kimataifa wa kuokoa maisha ukiwataja zaidi ya watu Milioni 10 wakiwa na mahitaji ya msaada huo.

Kulingana na O'Brien, nchi nyingine wanachama wa umoja wa Mataifa zimeahidi kutoa ahadi zao baadae mwaka huu, wakati Umoja huo ukiwa na matarajio ya kupata machango kutoka Marekani.

Ziara hiyo itaanzia Cameroun wiki moja baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutteres kuonya kuhusu kitisho cha njaa katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, ambako ni kitovu cha mzozo wa kundi la wapiganaji la Boko Haram.

Umoja wa Mataifa unahitaji kiasi cha Dola Bilioni 1.5 za msaada kwa mwaka huu wa 2017 katika Ukanda huo pekee. Angalau nusu ya kiasi hicho zinahitajika kwa ajili ya eneo la Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, ambako watu Milioni 5.1 wanakabiliwa na kitisho kikubwa upungufu wa chakula.

Kwenye ziara hiyo, wanadiplomasia hao wanatarajia kuzihimiza nchi hizo nne kuja na mikakati mipya ya kukabiliana na majanga amesema, balozi wa Ufaransa Fancois Delattre. amesema, serikali zinatakiwa kuandaa mbinu thabiti za kukabiliana na chimbuko la ugaidi, kwa kuhusisha masuala ya utawala na maendeleo.

Sweden ambayo si mwanachama wa kudumu wa Umoja wa Mataifa, na mfadhili mkubwa wa misaada ya kibinaadamu inatumaini baraza hilo litakuwa na nafasi muhimu zaidi ya kuutatua mgogoro huo.

Mwandishi: Lilian Mtono/APE/AFPE.
Mhariri:  Mohammed Abdul-Rahman