1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

Vita vya Ukraine vyaughubika mkutano wa wahisani wa Yemen

19 Machi 2022

Umoja wa Mataifa na makundi ya misaada wameonya kuwa hali inaweza kuwa mbaya sana nchini Yemen, baada ya mkutano wa wahisani kushindwa kuchangia fedha za kutosha kuzuia janga la kibinadamu katika taifa hilo lenye mzozo.

https://p.dw.com/p/48j9c
Ukraine Krieg | Jemens Hungerkrise und Lebensmittelpreise
Inflation
Sehemu kubwa ya raia wa Yemen huishi kwa kutegemea msaada kutoka nje ya nchiPicha: Khaled Abdullah/REUTERS

Kulingana na maelezo ya Umoja wa Mataifa, Yemen ambayo tayari inakumbwa na mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu iko kwenye ukingo wa kusambaratika, lakini imefunikwa na vita vinavyoendelea nchini Ukraine.

Soma zaidi: Umoja wa Mataifa watarajia kukusanya dola bilioni 4.27 kwa ajili ya Yemen

Umoja wa Mataifa umeelezea kuvunjwa moyo na matokeo ya mkutano wa wahisani uliofanyika Jumatano wiki hii, ambao uliambulia pungufu ya theluthi ya malengo yaliyokuwa yamewekwa ya kiwango cha fedha za msaada kwa ajili ya Wayemen 17.3 milioni walio na mahitaji ya dharura.

Ukraine Kiew | Mehrere Gebäude nach Angriffen zerstört
Uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine umeufunika mzozo wa Syria kwa njia mbali mbaliPicha: Andre Alves/AA/picture alliance

Yemen inategemea kwa kiasi kikubwa chakula na mahitaji mengine vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi, na mashirika ya msaada yana hofu kuwa hali itazidi kuzorota kutokana na mzozo wa Ukraine, nchi ambayo ni chanzo cha theluthi moja ya ngano inayosambazwa nchini Yemen.

Mgao kwa wenye mahitaji wapunguzwa kutokana na uhaba

Asilimia 80 ya raia wa taifa hilo la Kiarabu wapatao milioni 30 hutegemea msaada kwa maisha yao ya kila siku, baada ya vita vya miaka saba saba ambavyo athari zake zimeangamiza maisha ya mamia kwa maelfu ya watu.

Umoja wa Mataifa umesema mashirika ya misaada yanakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha kiasi kwamba yanalazimika kupunguza mipango yake ya kuokoa maisha ya watu.

''Upungufu huo maana yake ni kwamba hayatoweza kukidhi mahitaji ya watu wenye shida'', amesema Auke Lootsma, mwakilishi mkazi wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mipango ya Maendeleo, UNDP nchini Yemen.

Weltspiegel 01.03.2021 | Jemen Sanaa | Hunger | Kind mit Nahrungsergänzungs-Drink
Umoja wa Mataifa unaonya kuwa Wayemen wengi wanakabiliwa na baa la njaaPicha: Khaled Abdullah/REUTERS

''Matazamio ya mwaka ujao ni yenye kuvunja matumaini kwa Yemen. Huu ndio wakati mgumu zaidi tuliowahi kushuhudia katika nchi hii,'' aliongeza afisa huyo.

Madhila ya Yemen yanatokana na vita baina ya serikali inayotambuliwa kimataifa, ikiungwa mkono na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, na kundi la waasi wa Kihouthi linaloegemea upande wa Iran.

Hata kabla ya vita vya Ukraine hali ilikuwa mbaya

Shirika la chakula ulimwenguni, WFP limetoa tahadhari, likisema baa la njaa linaweza kufikia kiwango cha janga kadri mzozo wa Ukraine unavyosababisha kupanda kwa bei ya chakula.

Soma zaidi: UAE yaharibu kombora lililorushwa na waasi wa Kihouthi nchini Yemen

Lakini hata kabla ya uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, WFP imesema, tayari kiasi cha msaada wa chakula kwa Wayemen milioni nane kilikuwa kimepunguzwa, huku wapatao milioni tano tu wenye mahitaji ya dharura wakisalia katika orodha ya kupokea msaada kamili.

''Ni dhahiri kuwa wasiwasi unaoambatana na matukio nchini Ukraine umeugubika mkutano wa wahisani,'' amesema Abeer Atefa, msemaji wa WFP kuhusu ukanda wa Mashariki ya Kati, alipozungumza na shirika la habari la AFP.

Katika mkutano huo wa kukusanya msaada uliofanyika tarehe Machi 16, 2022, Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada ya kibinadamu walikuwa wakitarajia dola bilioni nne, lakini ziliahidiwa dola bilioni 1.3 ambazo hazifiki hata theluthi moja ya kiwango kilichokusudiwa.

afpe