1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Umoja wa Mataifa kuzikutanisha pande hasimu nchini Sudan

12 Desemba 2025

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanatarajiwa kukutana mjini Geneva na pande zinazohasimiana nchini Sudan katika juhudi za kutafuta suluhu ya kisiasa kwa mgogoro unaoendelea nchini humo.

https://p.dw.com/p/55CIi
Sudan al-Dabbah 2025 | Abdel Fattah al-Burhan
Jenerali wa jeshi la Sudan Fattah al-Burhan akizuru moja ya kambi za wakimbizi ya Al-AfadhPicha: Stringer/Anadolu Agency/IMAGO

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanatarajiwa kukutana mjini Geneva na pande zinazohasimiana nchini Sudan.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameliambia shirika la Habari la Al Arabiya la Saudi Arabia kuhusu mkutano huo, ingawa hakufichua tarehe ya mazungumzo hayo.

Guterres amesema Umoja wa Mataifa umehakikishiwa kuwa njia za kuingia mji wa El-Fasher ambao bado umekatwa mawasiliano, zitafunguliwa hivi karibuni, huku RSF ikiendelea kudhibiti upatikanaji wa huduma za intaneti na setilaiti za Starlink.

Matumaini ya kupatikana kwa mwanga katika mazungumzo kuhusu vita vya Sudan yaliongezeka mwezi uliopita baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kueleza utayari wa kusaidia kuumaliza mzozo huo kufuatia ombi la mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia Mohammed Bin Salman wakati wa ziara yake mjini Washington.

Tangu mnamo Aprili mwaka 2023, jeshi la Sudan na kikosi cha wanamgambo wa RSF vimekuwa vikipigana na kusababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwafanya takriban watu milioni 12 kuyahama makaazi yao.