1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya kukabiliana na teknolojia ya akili bandia

Daniel Gakuba
6 Juni 2023

Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya imezitaka kampuni zenye majukwaa makubwa ya kimtandao, kuziwekea alama maalumu vidio, sauti na maandishi vilivyotengenezwa kwa kutumia akili bandia.

https://p.dw.com/p/4SGAt
Symbolbild Smartphone & Apps
Picha: Yui Mok/empics/picture alliance

Makampuni hayo ya teknolojia ya mtandao, yakiwemo Google, Facebook, Youtube na TikTok yametakiwa kubaini picha, video na maandishi vilivyotengenezwa kwa njia ya akili bandia, na kuviwekea alama inayoonekana vyema ili watumiaji wavitambue.

Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Umoja wa Ulaya kupambana na taarifa za kupotosha, ambazo maafisa wa umoja huo wamesema zimeongezeka sana wakati huu wa vita vya Urusi dhidi ya Ukraine.

Umoja huo wenye makao yake mjini Brussels unahofu kuwa teknolojia ya akili bandia inaweza kuwa ardhi yenye rutuba ya kukuza taarifa za kupotosha na habari za uongo. Naibu Rais wa Umoja wa Ulaya Vera Jourova amesema programu za akili bandia ya hali ya juu kama ChatGPT kwa muda wa sekunde chache tu zinaweza kuunda vidio, sauti na picha ambavyo mtumiaji hawezi kuvitofatisha na vile vilivyo halisi. ''Programu hizo zinaweza kutengeneza picha inayoonekana halisi kabisa, juu ya jambo ambalo halikutokea. Programu za sauti zinaweza kuigiza sauti ya mtu kwa kutumia sampuli za mtu huyo. Teknolojia hii mpya inaleta changamoto mpya katika mapambano dhidi ya taarifa za uongo.''

Chat GPT
Programu mpya ya Chat GBT Picha: Nikos Pekiaridis/NurPhoto/picture alliance

Akizungumza mwanzoni mwa wiki hii, Jourova alitahadharisha juu ya kuenea kwa ripoti ya upotoshaji za Urusi katika nchi za kati na mashariki mwa Ulaya, na kuongeza kuwa mashine hazina haki ya uhuru wa kauli.

Hata hivyo, kampuni hizo za mtandaoni hazilazimiki kutekeleza agizo la Umoja wa Ulaya la kuziwekea alama maalumu kazi zilizoundwa kwa kutumia teknolojia ya akili bandia, bali ni suala la hiari yao kufanya hivyo, na hakuna adhabu yoyote ikiwa zitakaidi. Na vile vile, kama anavyobainisha Andrea Renda ambaye ni mtafiti mkuu wa masuala ya uchumi wa kidigitali katika kituo cha mambo ya Ulaya, kuna vikwazo vingi wa kiteknolojia.

Renda ameiambia DW kuwa hakuna uhakika wa asilimia 100 kwamba kampuni hizo zinaweza kung'amua kuwa sauti au picha imetokana na teknolojia ya akili bandia, na kuongeza kuwa hata kama kampuni hizo zitafuata maagizo ya Umoja wa Ulaya, itakuwa ni kuonyesha nia njema tu.

Lakini, Naibu Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Vera Jourova amesema alihakikishiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Google, Sundar Pichai, kwamba wametengeneza teknolojia yenye uwezo wa kuwajulisha watumiaji kuwa mauadhui wanayoyaona au kuyasikia hayakuundwa na binadamu.

TikTok inakabiliwa na vizuizi zaidi, nini kitarajiwe?

Twitter, kampuni ya mtandao wa kijamii inayomilikiwa na bilionea Elon Musk haikuwakilishwa katika kikao cha mjini Brussels cha kupambana na habari za upotoshaji, kwa sababu ilijiondoa katika mpango wa Umoja wa Ulaya kuhusu jambo hilo. Naibu Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya ameikosoa kampuni hiyo, akisema itafuatiliwa kwa karibu.

''Twitter imechagua njia ya mikwaruzano. Hilo limebainika katika Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, ingawa najua kuheshimu kanuni ni hiari. Lakini, hakuna shaka, kwa kuzikataa kanuni zetu, Twitter imejianika kweupe na matendo yake yatachunguzwa kwa makini ikiwa yanaheshimu sera za Umoja wa Ulaya.''

Chini ya sera za Umoja wa Ulaya, kampuni zote za teknolojia ya mtandao, Twitter ikiwemo, zitalazimika kuchunguza maudhui zinayoyachapisha kuanzia mwezi Agosti.

Sera hiyo ya udhibiti wa mitandao inayataka kampuni husika kuwa zenye uwazi juu ya teknolojia zinayoitumia, na kuimarifa michakato ya kuzichuja taarifa zenye madhara, na kupiga marufukumatangazo ya biashara yenye maadhui yanayohusiana na masuala tete kama dini mwelekeo wa watu kimapenzi.