Ujumbe wa Afghanistan washambuliwa na Taliban | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.03.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ujumbe wa Afghanistan washambuliwa na Taliban

Wanamgambo wa Taliban wameufyatulia risasi ujumbe wa serikali ya Afghanistan uliokuwa ukizuru mojawapo ya vijiji viwili kusini mwa nchi hiyo ambako mwanajeshi wa Marekani anashukiwa kuwauwa raia 16 wa Afghanistan.

An Afghan soldier speaks to civilians gathered outside a military base in Panjwai, Kandahar province south of Kabul, Afghanistan, Sunday, March 11, 2012. Afghan President Hamid Karzai says a U.S. service member has killed more than a dozen people in a shooting including nine children and three women. Karzai called the attack Sunday an assassination and demanded an explanation from the United States. He says several people were also wounded in the attack on two villages near a U.S. base in the southern province of Kandahar. (Foto:Allauddin Khan/AP/dapd)

Reaktionen nach dem Amoklauf in Kandahar

Ujumbe huo ulikuwa ukizungumza na familia za waathiriwa wa tukio la mauaji yaliyotokea Jumapili, katika kijiji cha Balandi wakati waliposikia milio ya risasi. Qayum Karzai, kaka yake Rais wa Afghjanistan Hamid Karzai ambaye alikuwa sehemu ya kundi hilo alisema haamini kuwa kuna yeyote aliyeuwawa katika mashambulizi hayo, lakini alisikia ripoti za mtu mmoja kujeruhiwa mguuni. Lakini kuna ripoti kuwa mwanajeshi mmoja wa Afghanistan ameuwawa katika tukio hilo.

Aliongeza kuwa maafisa wa ujumbe huo wako salama na kwamba wamerejea katika mji wa Kandahar. Mwandishi wa habari wa shirika la AP aliyekuwa katika ujumbe huo, alisema milio hio ya risasi ilitokea kutoka seehmu mbili tofauti.

Mshukiwa wa mauaji yuko kizuizini

Marekani inamzuilia mwanajeshi anayeshukiwa kuyafanya mauaji hayo kabla ya Alfajiri Jumapili katika vijiji viwili vilivyo karibu na kambi yao ya wilaya ya Panjwai mkoani Kandahar. Eneo hilo linachukuliwa kuwa ngome ya Taliban. Tisa kati ya 16 waliouwawa ni watoto na watatu walikuwa wanawake kulingana na Karzai.

Rais wa Marekani Barrack Obama alielezea kushtushwa kwake na huzuni na akatuma risala za rambirambi kwa familia za waathiriwa. Lakini pia amesema tukio hilo la kushtua haliwezi kuharakisha mipango ya kuviondoa vikosi vya kigeni nchini humo, licha ya ongezeko la upinzani nyumbani kuhusu vita vya Afghanistan.

Taliban yaapa kulipiza kisasi

Wanafunzi wa chuo kikuu mjini Jalalabad wamefanya maandamano

Wanafunzi wa chuo kikuu mjini Jalalabad wamefanya maandamano

Msemaji wa Taliban, Zabiullah Mujahid, aliapa kulipiza kisasi mashambulizi hayo. Alisema kupitia taarifa iliyotumwa kwa waandishi leo kwamba mwanajeshi huyo anayedaiwa kuua anafaa kushitakiwa kama mhalifu wa kivita na kisha kuuliwa na jamaa wa watu aliowauwa.

Aidha hii leo mamia ya wanafunzi Kaskazini mwa Afghanistan walipiga kele wakiishtumu serikali ya Marekani na mwanajeshi wa nchi hiyo anayedaiwa kufanya mauaji hayo, maandamano ambayo ni ya kwanza kuwahi kufanywa kujibu balaa hilo.

Wanafunzi waandamana Jalalabad

Mauaji hayo yamezua hasira nchini Afghanistan lakini hayajaibua maandamano ya ghasia kama yalivyoshuhudiwa mwezi uliopita baada ya wanajeshi wa Marekani kuchoma moto nakala za Kuran na nakala za vitabu vyengine vya dini ya Kiislamu.

Wanafunzi hao wa chuo kikuu cha mjini Jalalabad, kilomita 125 Mashariki ya mji mkuu Kabul, walipewa idhini ya kufanya maandamano hayo. Walichoma moto kibonzo cha Rais Barrack Obama. Walisema Umoja wa Mataifa na serikali ya Afghanistan zinafaa kumshtaki hadharani mshukiwa wa mauaji hayo.

Mwandishi: Bruce Amani/AP

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com