1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawazri wa mambo ya ndani kukutana Brussels

Admin.WagnerD14 Septemba 2015

Ujerumani hii leo imeanza utekelezaji wa utaratibu wa kukagua hati za kusafiria katika mpaka wake na Austria kufuatia kuendelea kumiminika kwa wakimbizi wanaotafuta hifadhi ya kisiasa nchini humo.

https://p.dw.com/p/1GWA9
Sehemu ya wakimbizi wanaoingia nchini Ujerumani.
Sehemu ya wakimbizi wanaingia nchini Ujerumani.Picha: DW/M. Gopalakrishnan

Hatua hiyo inakuja mnamo wakati idadi ya wakimbizi ikizidi kuongezeka nchini Hungary kuelekea mkutano wa mataifa yanayounda Umoja wa Ulaya wenye lengo la kujadili suala hilo.

Uamuzi huo uliotolewa na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel wa ukaguzi wa hati za kusafiria mipakani unafungua ukurasa mpya miongoni mwa mataifa hayo ya Umoja wa Ulaya kuhusiana na makubaliano yanayotoa uhuru wa kusafiri katika mataifa wanachama wa eneo la Schengen.

Wakati hayo yakiendelea Serikali ya Hungary imesema imepokea kiasi cha wakimbizi wapatao 5,809 wanaoingia nchini humo kabla ya utekelezaji wa sheria zake mpya kuhusiana na wahamiaji kuanza kutumika.

Hungary yakamilisha ujenzi wa uzio mpakani kudhibiti wakimbizi

Hungary kwa sasa inapambana kukamilisha ujenzi wa uzio wake wa senyenge mpakani ifikapo hapo kesho ili kudhibiti wakimbizi hao ambapo itaanza kuwatia mbaroni wahamiaji wanaoingia nchini humo kinyume cha sheria.

Waziri mkuu wa Hungary Victor Orban
Waziri mkuu wa Hungary Victor OrbanPicha: Reuters/B. Szabo

Dakika tano baada ya Ujerumani kuanza utaratibu wa ukaguzi wa hati za kusafiria askari polisi waliwazuia vijana wahamiaji watatu waliokuwa wakikimbia vita nchini Syria na kuanza kukagua hati zao za kusafiria.

Mawaziri wa mambo ya ndani kutoka katika mataifa yanayounda Umoja wa Ulaya wanatarajia kukutana hii leo jijini Brussels ili kujaribu kupunguza tofauti zilizopo miongoni mwa mataifa hayo hivi sasa kuhusiana na mgogoro huo wa wakimbizi ambao ni mkubwa zaidi tangu kumalizika kwa vita kuu vya pili vya dunia.

Ujerumani ambayo inatarajia kupokea wakimbizi 800,000 mwaka huu awali ilikuwa imefungua milango yake kwa wakimbzi kutoka nchini Syria lakini kauli ya sasa ya taifa hilo lenye uwezo mkubwa wa kiuchumi barani Ulaya inaashiria umuhimu wa kikao hicho cha mawaziri wa mambo ya ndani kinachofanyika Brussels .

Halmashauri ya Umoja wa Ulaya juma lililopita ilizindua mpango wa kugawanya idadi ya wakimbizi 160,000 miongoni mwa mataifa hayo ili kuzipunguzia mzigo nchi za Italia, Ugiriki na Hungary. Hata hivyo mpango huo unaonekana kutoungwa mkono na mataifa ya Ulaya mashariki yakiwemo Jamuhuri ya Czech na Slovakia.

Wakati huohuo waziri mkuu wa Uingereza David Cameron hii leo ametembelea kambi ya wakimbizi wa Syria iliyoko mashariki mwa Lebanon na kuzungumza na wakazi wa eneo hilo. "Nilitaka kuja hapa ili kujionea na kusikia mwenyewe taarifa za wakimbizi na nini wanachohitaji" Cameron alikieleza kituo cha televisheni cha Uingereza wakati alipokuwa akiendelea kutembea kambi hiyo.

Waziri mkuu huyo wa Uingereza ametembelea kambi ya Torbol mashariki mwa Lebanon iliyo na wakimbizi 600 wa Syria baada ya kuwasili Beirut.

Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE/DPAE

Mhariri: Iddi Ssessanga