Ugiriki yenye madeni yapata pigo jipya
20 Septemba 2011Mkutano uliofanywa jana usiku kwa njia ya simu pamoja na Umoja wa Ulaya, Benki Kuu ya Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF, ulimalizika bila ya mafanikio makubwa.
Hata hivyo, Waziri wa Fedha wa Ugiriki, Evangelos Venizelos amesema, mazungumzo hayo yalikuwa na manufaa na umuhimu. Lakini bado kuna kazi kadhaa za kutekelezwa. Kwa mujibu wa Umoja wa Ulaya, leo jioni pia kutafanywa mkutano mwingine kwa njia ya simu.
Wakati huo huo, vyombo vya habari vinasema, serikali ya Ugiriki imepewa orodha ya hatua 15 zinazopaswa kutekelezwa haraka ili kubana matumizi. Ripoti ya wafadhili ndio itakayosaidia uamuzi kupitishwa, iwapo Ugiriki ipewe Euro bilioni 8 kutoka mfuko wa Euro bilioni 110. Habari rasmi zinasema, Ugriki inahitaji fedha hizo kwa dharura, ama sivyo itashindwa kukidhi gharama zake katika mwezi wa Oktoba.
Wakati huo huo, Rais wa Benki ya Dunia, Robert Zoelleck ameonya kuwa mzozo wa madeni wa nchi tajiri zilizoendelea kiviwanda, vile vile unaathiri nchi zinazoinukia kiuchumi na zinazoendelea. Zoelleck, amesema, tayari kuna dalili za mwanzo katika masoko ya hisa na fedha. Akizungumza kabla ya kufunguliwa mkutano wa mwaka wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF, mjini Washington, Zoelleck amesema, hivi sasa nchi zinazoinukia hazina uwezo wa kujikinga dhidi ya mzozo mpya wa kiuchumi. Ametoa mwito kwa nchi tajiri kuushughulikia kwa pamoja mzozo wao wa madeni.
Mada kuu katika mkutano huo wa mwaka, ni madeni makubwa ya baadhi ya nchi za Ulaya na hatari ya ukuaji wa kiuchumi kupungua kote duniani