Ugiriki wahaha kuzuia uchaguzi mpya
15 Mei 2012Ugiriki imejikuta katika mkwamo kuhusiana na mpango wa kubana matumizi ambao unapingwa vikali na vyama vidogo nchini humo, na hivyo kuweka mustakabali wa taifa hilo katika kanda ya euro mashakani.
Kiongozi wa chama cha kisoshalsti cha Pasok, Evangelos Venizoelos, alisema viongozi wa vyama vyote vilivyopata uwakilishi katika uchaguzi wa Mei 6, ukiacha kile chenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia, walikutana kujaribu kufikia mwafaka na kuzuia kurudiwa kwa uchaguzi.
Ugiriki inanyemelewa na uchaguzi mpya endapo siku ya Alhamis itafika na hakuna serikali, jambo ambalo litazidi kuiweka katika hali mbaya zaidi kiuchumi kutokana na kusimama kwa biashara kati yake na mataifa mengine katika kanda inayotumia sarafu ya euro na pia masoko ya fedha.
Rais Carolos Papoulias alikutana na Venizelos na kiongozi wa chama cha kihafidhina cha New Democracy na yule wa chama cha mrengo wa kushoto cha Syriza na kupendekeza iundwe serikali inayoongozwa na wataalamu wasio wana siasa, kama vyama hivyo vitashindwa kufikia makubaliano, akiongeza kuwa muda ulikuwa unawatupa mkono.
Mitihani inayoikabili Ugiriki
Tayari mtihani wa kwanza kwa taifa hilo ulikuja siku ya Jumanne wakati wa mauzo ya hati ya mkopo wa serikali ambayo yanafuatiliwa kwa karibu sana baada ya masoko ya fedha ya Ulaya kuyumba hapo siku ya Jumatatu kufuatia habari kuwa mgogoro wa madeni ya kanda ya euro unaweza kuikwamisha Hispania au hata Italia.
Ugiriki ilifaulu mtihani mwingine siku ya Jumanne baada ya kufanikiwa kulipa madeni ya kiasi cha euro milioni 436 kwa wakopeshaji binafsi ambao hapo awali walikuwa wamegoma kushiriki mpango Umoja wa Ulaya na IMF uliyowataka wakubali kupata hasara kwenye mikopo yao, kama sharti la kuokolewa kwa Ugiriki huko nyuma.
Idadi ndogo ya wakopeshaji binafsi iliukataa mpango huo na kutishia kwenda mahakani ili kurejesha fedha zao, na chanzo cha habari kilisema hatu hii ya kulipa deni hili ilikuwa inalenga kuzuia mgogoro mwingine.
Kura ya hasira
Katika uchaguzi wa Mei 6 wapiga kura walipiga kura ya hasira dhidi ya masharti magumu ya mpango huo wa uokozi ambao serikali ya awali iliyokuwa inaongozwa na Waziri Mkuu Lucas papademos iliyakubali ili kupatiwa kiasi cha Euro bilioni 240 kuokoa uchumi wa nchi hiyo uliokaribia kuanguka kabisaa.
Katika miezi ya hivi karibuni, maafsia wa Umoja wa Ulaya wamekuwa wakizungumzia uwezekano wa Ugiriki kuondoka katika kanda ya sarafu ya Euro, lakini siku ya jumatatu kiongozi wa mawaziri wa fedha wa kanda hiyo, Jean Claud Juncker, alipuuza mawazo hayo.
"Matumaini yetu ni kuibakiza Ugiriki katika kanda ya Euro na tutafanya kila liwezekanalo kutimiza hilo," alisema Juncker.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\AFPE
Mhariri: Othman Miraji