Ugiriki katika madeni | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.03.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ugiriki katika madeni

Waziri mkuu wa Ugiriki atakutana ijumaa na Merkel kutafuta njia ya kupata msaada

default

Waziri mkuu wa Ugiriki George Papandreou asema nchi yake haihitaji msaada wa fedha wa Ujerumani

Ugiriki imesema haihitaji msaada wa fedha kutoka Ujerumani badala yake inataka kuungwa mkono kisiasa.Kwa maneno mengine waziri mkuu wa Taiafa hilo George Papandreou amesema Ugiriki hailazimiki kulipa kiwango kikubwa cha riba kwa ajili ya kupata mkopo. Matamshi hayo ya Ugiriki yamekuja wakati ambapo Kesho waziri mkuu huyo atakutana na Kansela Merkel mjini Berlin kwa lengo la kujadiliana jinsi ya kulitatua tatizo hilo.

Tayari imearifiwa kwamba katika mkutano huo utakaofanyika kesho mjini Berlin Kansela Angela Merkel wa Ujerumani anatarajiwa kumueleza wazi waziri mkuu wa Ugiriki kwamba wagiriki wanabidi kuyatatua wenyewe matatizo yao ya kiuchumi.Waziri wa Uchumi wa Ujerumani Rainer Bruederle amesikika akisema kwamba Ujerumani inabidi izingatie sheria kwamba kila nchi barani Ulaya inatakiwa kuyatatua na kusimamia matatizo yake yenyewe.

Ujerumani kama taifa lenye uwezo mkubwa wa kiuchumi barani Ulaya linaangaliwa kwa kiasi kikubwa kama nchi ya kwanza itakayolazimika kujitolea kuipa Ugiriki msaada wa fedha wa kujikwamua katika matatizo ya kiuchumi.Hata hivyo hilo halitofanyika kutokana na kuwa wajerumani wengi wanaipinga hatua kama hiyo jambo ambalo limemfanya kansela Angela Merkel kubakia na msimamo wa waliowengi nchini wa kukataa kuisadia Ugiriki na kusema kwamba kila mtu abebe msalaba wake.

Hata hivyo kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari serikali ya mjini Berlin inatafuta mipango chinichini ikiwa ni pamoja na aidha mpango wa mataifa mawili kuisadia Ugiriki au Umoja wa Ulaya kama kundi moja kuungana na kuchukua hatua au kuisaidia kupitia shirika la fedha duniani IMF. Hapo jana Ugiriki ilitangaza mpango wake wa mabilioni ya euro wa kujihini kwa kipindi cha miezi kadhaa na ambao unalenga kupunguza bajeti na madeni yake pamoja na kuwashawishi wawekezaji waendeleaa kubakia katika taifa hilo.Akiuzungumzia mpango huo kasnela Angela Merkel wa Ujerumani hapo jana alisema kwamba anaunga mkono hatua hiyo ya Ugiriki na zaidi ya hilo-

''Naamini kwamba hakuna njia nyingine ya kufuata kwa Ugiriki,inabidi ishughulikie tatizo hili.Nimefurahi na nimeridhika kwamba serikali ya Ugiriki na waziri mkuu wa taifa hilo hawaogopi kuchukua juhudi zozote za kutatua tatizo hili na badala yake wameamua kufuata njia isiyoweza kuepukwa.''

Wakati kukiwa na wasiwasi juu ya uwezo wa kifedha wa Ugiriki katika kushughulikia madeni yake ambayo yanasababisha kulisukuma eneo linalotumia sarafu ya Euro katika mzozo mkubwa wa kiuchumi,waziri mkuu wa Ugiriki kesho atafanya mazungumzo na Kansela Merkel na kutafuta mkakati wa kuisadia nchi hiyo. Jumapili waziri huyo pia amepangiwa kukutana na rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa.Kabla ya hapo jana Ugiriki kutangaza mpango wake wa kujihini Papandreou alisema kwamba ikiwa watashindwa kupata msaada wa Umoja wa Ulaya inaweza kuomba msaada huo kwa shirika la fedha duniani IMF jambo ambalo litakuwa ni aibu kubwa kwa Umoja huo wa Ulaya ambao ni mshirika wa Ugiriki.

Mwandishi Saumu Mwasimba/DPAE

Mhariri Othman Miraji.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com