1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Uhuru wa vyombo vya habariUganda

Uganda yawapa masharti magumu waandishi wa habari

13 Januari 2026

Tume ya uchaguzi na vyombo vya usalama nchini Uganda vimetoa masharti kwa wanahabari watakaoandika na kusambaza habari za uchaguzi. Miongoni mwa masharti hayo ni kutowahoji waangalizi na kutangaza matokeo yasiyo rasmi.

https://p.dw.com/p/56l7j
Uganda Kampala 2026 | Bobi Wine akiwa na wafuasi wa chama cha NUP wakati wa mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi
Kiongozi wa upinzani nchini Uganda na mgombea urais wa (NUP) Robert Kyagulanyi Ssentamu, maarufu kama Bobi Wine (C), akipeperusha bendera sambamba na wafuasi alipowasili kwenye mkutano wa mwisho wa kampeni za chama hicho kabla ya uchaguzi mkuu wa 2026, jijini Kampala mnamo Januari 12, 2026.Picha: Luis Tato/AFP/Getty Images

Leo ndiyo siku ya mwisho ya kampeni za uchaguzi na tume ya uchaguzi imetoa masharti kwa wanahabari ikisema kuwa lengo ni kuhakikisha kuwa taarifa zinazofikia umma ni rasmi na wala hazichochei watu.

Akihutubia wandishi habari kabla ya kuwakabidhi rasmi vitambulisho vyao, mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Jaji Simon Byabakama ameonya kuwa mwanahabari yeyote ambaye atakiuka kanuni husika atakuwa hatarini kuchuykuliwa hatua ambazo zitastahili kama adhabu kwake yeye na shirika la habari analowakilisha.

Sharti la kwanza limekuwa kwamba kila mwanahabari apate idhini kutoka kwa Baraza la Waandishi habari na kupewa kibali cha kuendesha shughuli zake. Ni kwa msingi huu ndipo amekabidhiwa kitambulisho. 

Wanahabari wa kimataifa wamepitia mchakato mrefu zaidi wa kuchujwa na baraza la wanahabari pamoja na vyombo vya usalama kabla ya kuruhusiwa kuendesha shughuli zao. Mara nyingi haki za wanahabari zikikiukwa, wao hukimbilia kwa mtandao wa kupigania haki za wanahabari HRJN.

Jeshi la Uganda linavyojihusisha kwa karibu na uchaguzi mkuu

Lakini shirika hilo limesitishwa shughuli zake na mamlaka inayosimamia mashirika yasiyo ya serikali hapo jana kwa madai kwamba baadhi ya shughuli zake zinahatarisha usalama wa taifa Mashirika mengine manne pia yamefunguwa shughuli zao kwa sababu hiyo hiyo huku ikisemekana kuwa uchunguzi dhdi yao unaendelea.

Changamoto nyingine ambayo wanahabari wanatarajia itakuwa kikwazo kwao kufanya kazi zao ni kama serikali itaamua kuzima mitandao ya intaneti. Hili limekuwa jambo la kawaida katika kipindi cha uchaguzi na tangu mwaka 2021 jukwaa la Facebook lingali marufuku kutumiwa

Wasemaji wa vyombo vya usalama wametoa onyo kali kwa wanahabari kutii maagizo yoyote watakaopewa na askari jeshi au polisi wakati wa uchaguzi. Wametahadharisha kuwa hawatasita kuwachukulia hatua ikiwemo kuwakamata na kuwazuilia hasa wakionekanakuchochea wananchi.

Wandishi habari hasa wale ambao wamekuwa wakimfuatilia mpinzani mkuu wa kiti cha urais, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, wamejikuta katika wakati mgumu zaidi.