1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufisadi Kenya: Mihimili mitatu ya serikali yapewa siku 30

Shisia Wasilwa
22 Januari 2024

Mihimili mitatu ya serikali nchini Kenya zina siku 30 za kuandaa mapendekezo ya namna ya kukabiliana na ufisadi.

https://p.dw.com/p/4bYP4
Kenya, William Ruto
Rais William Ruto wa KenyaPicha: Dominika Zarzycka/NurPhoto/picture alliance

Kwenye mkutano wa faragha katika ikulu ya Nairobi kati ya Rais William Ruto, Jaji Mkuu Martha Koome, na Spika wa Bunge Moses Wetangula, ilikubaliwa kuwa mihimili hiyo mitatu ingeliwasilisha mapendekezo hayo kwa Baraza la Taifa la Kutekeleza Haki kwa lengo la kumaliza mvutano kati ya serikali ya Ruto na Mahakama kuhusu madai ya rushwa dhidi ya majaji kwa manufaa ya wananchi. 

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, viongozi kwenye mihimili hiyo mitatu ya serikali waliafikiana kuunda sera, miongozo na kanuni na miswada ili kuyafanikisha malengo yao.  

Mkutano huo wa siku ya Jumatatu (Januari 22) huenda ukapunguza misuguano kati ya baraza la mawaziri chini ya Rais Ruto na Idara ya Mahakama ambayo imekuwa ikishuhudiwa katika kipindi kirefu cha mwaka huu.