Ufaransa yatangaza kisa cha Ebola nje ya bara Afrika
25 Juni 2026
Daktari mmoja aliyerejea nchini humo kutokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ndiye aliyegundulika na kirusi hicho. Kisa hicho ni cha kwanza kilichogunduliwa nje ya bara la Afrika wakati wa mlipuko wa sasa nchini Kongo, ambao pia umeathiri Uganda. Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesusameonya dhidi ya "kuchukua hatua kupita kiasi" kwa kisa hicho -- cha kwanza kugunduliwa nchini Ufaransa. Tedros amesema "hakuna haja ya hofu", akisisitiza kwamba "hatari ya ugonjwa huo kuenea ulimwengu wote ni ndogo". Hata hivyo, alisisitiza kwamba kisa hicho kinatumika kama "ukumbusho wa hatari zinazowakabili wahudumu wa dharura walio mstari wa mbele kukabiliana na mlipuko huo". Amesema karibu wafanyakazi wa afya 80 wameambukizwa, jambo linalodhihirisha hatari wanazokabiliana nazo na umuhimu wa kuimarisha kinga na udhibiti wa maambukizi.
Kisa hicho kilichothibitishwa Jumatano kilimhusisha daktari ambaye alikuwa akifanya kazi na Alliance for International Medical Action (ALIMA). Wizara ya afya ya Ufaransa ilisema mgonjwa huyo "alipanda ndege ya abiria kutoka Kinshasa na hakuonekana kuwa na dalili -- isipokuwa maumivu ya kichwa." Hali yake "ilizidi kuwa mbaya kidogo wakati wa safari na baada ya hapo walitengwa mara moja na kuanza kuhudumiwa walipotua Paris, hata kabla ya ugonjwa huo kutambuliwa rasmi. Yuko katika "hali imara" na kiwango chake cha virusi kilikuwa "chini sana".