Ufaransa yahalalisha ndoa za jinsia moja | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.04.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ufaransa yahalalisha ndoa za jinsia moja

Wabunge wa Ufaransa wameidhinisha mswada wa kuhalalalishwa kwa ndoa za jinsia moja licha ya upinzani mkali na kuifanya nchi hiyo kuwa ya 14 kote duniani kuhalalalisha ndoa za mashoga.

Wabunge wa Ufaransa hapo jana waliidhinisha mswada wa kuhalalalishwa kwa ndoa za jinsia moja licha ya upinzani mkali na kuifanya nchi hiyo kuwa ya 14 kote duniani kuhalalalisha ndoa za mashoga. Makabiliano makali yameripotiwa kati ya waandamanaji na maafisa wa polisi nchini humo.

Maandamano yashuhudiwa Ufaransa kupinga ndoa ya jinsia moja

Wanaopinga sheria hiyo wameapa kuendeleza mapambano yao ya kuupinga na tayari wameshawasilisha kesi kwa baraza la kikatiba kupinga huku wakiahidi kufanya maandamano zaidi kumshinikiza Rais wa Ufaransa Francois Hollande kutotia saini na kuufanya rasmi sheria.Hapo jana wabunge 331 waliupigia kura dhidi ya 225 ili kuruhusu ndoa za watu wa jinsia moja na kuwapa uwezo wa kuasili watoto.

Waziri wa haki na sheria nchini humo wa chama tawala cha kisosholisti Christinae Taubira alipongeza kuidhinishwa huko kwa mswada kama hatua ya kihistoria akisema inahakikisha haki na kupinga unyanyapaa hivyo basi kudhihirisha wazi uwezo wa nchi hiyo kutambua na kuheshimu ndoa.

Wabunge wa Ufaransa hapo jana waliidhinisha mswada wa kuhalalalishwa kwa ndoa za jinsia moja licha ya upinzani mkali na kuifanya nchi hiyo kuwa ya 14 kote duniani kuhalalalisha ndoa za mashoga. Makabiliano makali yameripotiwa kati ya waandamanaji na maafisa wa polisi nchini humo.

Maandamano mjini Paris kupinga kuhalalishwa kwa ndoa za mashoga

Hata hivyo hali ya taharuki ilitanda ndani na nje ya majengo ya bunge huku kukionekana kuwa na maafisa wengi wa polisi. Maseneta kutoka upande wa upinzani UMP na vyama vingine vya mrengo wa kulia wamesema maana ya ndoa haiwezi tu kutoholewa na sheria moja hasa kipengele kinachoruhusu mashoga kupata watoto wa kupanga kinakiuka misingi mikuu ya ndoa ikwemo hadhi na usawa wa binadamu.

Sheria yaibua hisia mseto

Maelfu ya waandamanaji wanaopinga sheria hiyo waliandamana usiku mzima nje ya majengo ya bunge na kuapa kamwe hawatachoka kuupinga.Baraza la kanisa katoliki nchini Ufaransa limeelezea masikitiko yake kwa kuidhinishwa kwa sheria hiyo.Askofu Bernard Podvin amesema demokrasia imetawala lakini sheria hiyo tete haiwezi kuleta mshikamano wa kijamii.

Msemaji wa kundi kuu la mashoga nchini humo Nicolas Gougain akisifu hatua hiyo ya bunge na kusema ni usawa na demokrasia kwani haimpokonyi mtu yeyote haki bali inawapa haki wengine kwa kuwapa uhuru baada ya miaka mingi ya kupigania usawa.

Mashoga wakionyesha ishara ya mapenzi kutaka kutambulika kisheria

Mashoga wakionyesha ishara ya mapenzi kutaka kutambulika kisheria

Katika wiki za hivi karibuni,kumekuwa na mashambulio makali dhidi ya mashoga na hata baadhi ya wabunge kupokea vitisho.Kumekuwa vile vile na misururu ya maandamano ambayo yameonekana kushika kasi na kupata uungwaji mkono hata kutoka kwa wale ambao awali walikuwa wakiunga mkono mahusiano hayo ya mashoga na kinachoonekana kuchochea hili ni kipengele cha wao kuweza kuchukua watoto wa kuasilia.

Wanaopinga ndoa hizo wanatumai kuwa wanaweza kumshinikiza vya kutosha Rais Hollande kutotia saini mswada huo na kuufanya sheria licha ya kuwa ndiye muungaji mkuu wa ndoa za jinsia moja.Takwimu nchini humo zinaonyesha kuwa watu laki mbili wamejitangaza kuishi na wapenzi wao wa jinsia moja.

Iwapo Hollande atatia saini mswada huo basi Ufaransa itajiunga na mataiafa mengine ya Ulaya yaliyohalalisha ndoa hizo ikiwemo Uholanzi,Ubelgiji,Uhispania,Norway,Sweden,Ureno,Iceland na Denmark.

Mwandishi: Caro Robi/Afp/ap

Mhariri:Iddi Ssesanga.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com