Ufadhili kwa siasa kikwazo kwa uwazi | Matukio ya Afrika | DW | 30.03.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Ufadhili kwa siasa kikwazo kwa uwazi

Licha ya tafauti za mifumo ya kifedha baina ya mataifa tafauti duniani, utafiti wa Taasisi ya Global Integrity unaonesha mataifa duniani yanalingana katika kushindwa kudhibiti kwa ufanisi fedha zinazoingia kwenye siasa.

Yuan

Yuan

Katika masuala ya uwezo wa kisheria kuratibu na kuhakiki michango ya watu binafsi na mashirika kwa vyama vya siasa, utafiti huo uliochapishwa leo unaonesha kuwa mataifa 29 kati ya 31 yaliyohusika, yalipata chini ya alama 60 katika alama 100 zilizowekwa.

Taasisi za kiserikali zilizowekwa kuhakikisha sheria hizo zinafuatwa, zinaripotiwa kutokuwa na nguvu za uchunguzi na mara nyingi huwa zina uwezo mdogo wa kuweka vikwazo au mara nyengine hazina kabisa.

Katika mataifa 31 yaliyofanyiwa kazi na kundi la Global Integrity, Kenya imepata alama sifuri katika 100 juu ya suala la ufanisi wa kanuni zake za uchangiaji vyama vya siasa, ambapo katika masuala ya sheria za jumla imepata alama 67 katika 100.

Kenya miongoni mwa mataifa yaliyofeli

Maandamano dhidi ya ufisadi China.

Maandamano dhidi ya ufisadi China.

Kenya pia imefanya vibaya eneo la uchangiaji wa fedha kwa wanasiasa binafsi, ambapo mfumo wa kisheria umepata alama 20 na alama 0 kwenye alama 100 katika utekelezaji. Utafiti huo umegundua kuwa uwekwaji hadharani wa taarifa za michango ya fedha kwa wagombea na vyama haupo kabisa, kwa kuweka alama 0 katika 100.

Mataifa mengine yaliyopata alama 0 kwenye eneo hili, ni pamoja na Burkina Faso, Sierra Leone na Zimbabwe kwa Afrika, Nicaragua kwa Amerika ya Kusini na China kwa bara la Asia.

Mkurugenzi Mtendaji wa Global Intergrity, Nathaniel Heller, amesema kwamba taasisi yake inatiwa wasiwasi sana na ukosefu wa maendeleo duniani katika suala la kudhibiti uingiaji kiwango kikubwa cha fedha kutoka vyanzo binafsi kwenye uchaguzi.

Ufisadi wasambaa

Rais Mwai Kibaki

Rais Mwai Kibaki

Heller amesema na hapa namnukuu: "Ufadhili wa kisiasa unabakia kuwa chanzo nambari moja ya ufisadi duniani kote, na kukosekana kwa mageuzi yenye maana, kutaendelea kuzuia miradi mingi ya kuifanya serikali kuwa wazi." Mwisho wa kumnukuu.

Utafiti huo uliokuwa ukitathmini tiba inayotumika dhidi ya ufisadi badala ya ufisadi wenyewe katika kiwango cha taifa, ulitathmini pia maeneo mengine ya uwazi na uwajibikaji wa serikali, zikiwemo sheria zenye mgongano wa maslahi, uhuru wa vyombo vya habari na uwajibikaji katika kudumisha utawala wa sheria.

Utafiti huu umezishirikisha nchi zilizoendelea, kama vile Marekani, Ireland na Ujerumani, zinazoinukia kiuchumi kama vile India na China na zinazoendelea kama vile Indonesia, Ghana, Uganda na Ukraine. Bila ya kugusia maeneo ya uelewa wa watu kuhusu ufisadi, ripoti ya utafiti huo iliyochapishwa leo, inatathmini nyenzo za uwajibikaji na hatua za uwazi zilizopo kuzuia ufisadi.

Mambo mengine yaliyogunduliwa ni utafiti huu ni pamoja na kushindwa kwa taasisi za kupambana na ufisadi na vyama tawala kuhodhi urasimu serikalini au kutumia nafasi zao serikalini kwa maslahi ya vyama hivyo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Global Intergrity
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman