1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Senegal kufanyika Juni 2

28 Februari 2024

Tume ya kusimamia mazungumzo ya kitaifa nchini Senegal imependekeza uchaguzi wa rais uliocheleweshwa ufanyike Juni 2, hatua inayoweza kuurejesha upya mzozo wa kisiasa ulioanza tangu pale Rais Macky Sall alipouahirisha.

https://p.dw.com/p/4czZy
Maandamano ya Senegal
Mmoja wa waandamanaji waliokuwa wanapinga kuahirishwa kwa uchaguzi wa Senegal mjini Dakar.Picha: John Wessels/AFP

Mjumbe mmoja watume hiyo, Ndiawar Paye, alisema siku ya Jumanne (Februari 28) kwamba tume hiyo imependekeza pia Rais Macky Sall abakie madarakani hadi mrithi wake atakapoapishwa. 

Mapendekezo hayo yalitolewa baada ya mazungumzo ya siku mbili yaliyoandaliwa na Rais Sall kutuliza mvutano, lakini ambayo yalisusiwa na wagombea wengi wa upinzani.

Soma zaidi: Rais wa Senegal atangaza msamaha kwa wafungwa wa kisiasa

Paye aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa mapendekezo hayo sasa yatawasilishwa kwa rais atakayefanya uamuzi wa mwisho.

Taifa hilo la Afrika Magharibi, ambalo linatarajia kuanza kuchimba mafuta na gesi ifikapo mwisho wa mwaka huu, lilitumbukia kwenye mzozo wa kisiasa, baada ya Rais Sall kuahirisha uchaguzi uliopangwa kufanyika Februari 25.