Ubelgiji yairarua Estonia 8-1
14 Novemba 2016Ubelgiji iliikandika Estonia mabao 8-1 na kujiweka juu kabisa ya kundi H katika kinyang'anyiro cha kuwania kukata tikiti ya kucheza katika fainali za kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi, wakati Cristiano Ronaldo alipachika mabao mawili wakati Ureno ikichomoka katika kitisho cha Latvia kabla ya kuirarua timu hiyo kwa mabao 4-1 katika mchezo wa kufuzu kukata tikiti ya kucheza katika fainali za kombe la dunia jana Jumapili.
Kwa upande wa Ubelgiji Romelo Lukaku na Dries Mertens walifunga mabao ikiwa ni pamoja na Thomas Meunier , Eden Hazard , Yannick carrasco pamoja na goli la kujifunga wenyewe na kupata ushindi mara nne katika michezo minne.
Katika kundi hilo hilo Ugiriki ilipata bao la kusawazisha katika dakika ya 95 kupitia kwa Giorgos Tzavellas baada goli la kuongoza la Bosnia.
Pointi moja ya Ugiriki ina maana kwamba Wagiriki sasa wana pointi 10 kutokana na michezo minne katika kundi H, mbili nyuma ya Wabelgiji.
Ronaldo alifunga mabao mawili akakosa penalti wakati mabingwa wa Ulaya Ureno wakibakia pointi tatu nyuma ya viongozi wa kundi B , Uswisi. Mapema katika kundi hilo B Visiwa vya Faroe walishindwa kuhimili vishindo vya Uswisi kwa kukandikwa mabao 2-0.
Katika kundi hilo pia Hungary iliishindilia Andora kwa mabao 4-0.
Uholanzi iliishinda Lexemburg kwa mabao 3-1 katika kundi A, wakati pia katika kundi hilo Bulgaria ilikaba koo Belarus kwa kuifunga bao 1-0.
Mwandishi: Sekione Kitojo
Mhariri: Yusuf Samu