Ubalozi wa Marekani wahamishiwa Jerusalem kutoka Tel Aviv | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.05.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ubalozi wa Marekani wahamishiwa Jerusalem kutoka Tel Aviv

Ubalozi wa Marekani nchini Israel unahamishiwa Jerusalem, kufuatia tangazo la Rais Donad Trump la kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa taifa hilo. Ni hatua iliyokosolewa kimataifa, na kuwaghadhibisha Wapalestina.

Serikali ya Israel imeipongeza hatua ya Trump, kwa kusema kwamba imeutambua uhusiano kati ya historia ya Kiyahudi na mji huo mtakatifu wa Jerusalem. Wakati huo huo, Mamlaka ya ndani ya Palestina ambayo inadai Jerusalem Mashariki utakuja kuwa mji mkuu wa taifa lao la baadaye la Palestina, imekasirishwa na hatua hiyo ya Trump.

Katika hafla ya uzinduzi wa ubalozi huo wa Marekani mjini Jerusalem, iliyofanywa jana na Israel Waziri Mkuu wa taifa hilo, Benjamin Netanyahu amezitaka nchi nyingine kufuata mfano wa Marekani.

"Nazitolea wito nchi zote kuungana na Marekani na kuzihamishia balozi zao mjini Jerusalem. Hamishieni balozi zenu Jerusalem kwa sababu ni hatua itakayoleta amani. Amani inajegwa kwa msingi wa ukweli. Na ukweli ni kwamba Jerusalem umekuwa mji mkuu wa Wayahudi kwa milenia na ni mji mkuu wa taifa letu tokea lilipoanzishwa. Ukweli ni kwamba chini ya makubaliano yoyote ya amani ambayo unaweza kuyafikiria, Jerusalem utabaki kuwa mji mkuu wa Israel," amesema benjamin Netanyahu.

Desemba iliyopita, Rais Donald Trump alitangaza kwamba ubalozi wa Marekani utahamishwa kutoka Tel Aviv na kupelekwa Jerusalem, akiwa anatimiza ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2016. Uamuzi wake huo ulikosolewa duniani kote. Makubaliano ya jumuiya ya kimataifa ni kwamba suala la Jerusalem linapaswa kuwa sehemu ya majadiliano ya mwisho ya amani kati ya Israel na Palestina.

Marekani: kuhamishwa ubalozi hakuipi Israel mamlaka ya Jerusalem

Utawala wa Trump umesema tangazo lao halimaanishi kuwa Israel ina uhuru wa mji mzima, lakini Wapalestina wameiangalia hatua hiyo kuwa inaunga mkono udhibiti wa Israel wa mji mzima.

Mamlaka ya Palestina imekemea vikali uamuzi wa serikali ya Trump kuhusu mji huo wa Jerusalem na imekataa kukutana na maafisa wowote wa Marekani tokea wakati huo. Palestina imezitaka nchi nyingine kususia kuhudhuria uzinduzi rasmi unaofanyika leo jioni katika ubalozi wa Marekani, ambao utahudhuriwa na takriban watu 1,000, miongoni mwao ujumbe wa Marekani utakaoongozwa na waziri wa fedha Steven Mnuchin. Binti wa Trump Ivanka pia atahudhuria hafla hiyo.

Wapalestina wanaoishi katika Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza wamepanga kufanya maandamano ya kupinga kuhamishwa huko kwa ubalozi wa Marekani.

Israel ililiteka eneo la mashariki mwa Jerusalem mnamo mwaka 1967 kutoka Jordan, wakati wa vita kati ya nchi za Kiarabu na Israel. Ni hatua ambayo haikuwahi kutambuliwa kimataifa. Mnamo mwaka 1980, Israel ililitwaa eneo la Jerusalem Mashariki na kuutangaza mji mzima kama mji wake mkuu. 

Uamuzi wa Marekani unatazamwa kama unaopuuza uwepo wa Wapalestina pamoja na mafungamano ya kihistoria waliyo nayo na mji huo wa kale, ambao ni mtukufu kwa Waislamu, Wayahudi na Wakristo.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/dw/dpa

Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com