Tshisekedi aahidi kusuluhisha tatizo la uraia wa nchi mbili | Matukio ya Afrika | DW | 26.04.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Tshisekedi aahidi kusuluhisha tatizo la uraia wa nchi mbili

Rais wa DRC, Félix Tshisekedi amesisitiza kujitolea kwake ili kutatua suala la uraia wa nchi mbili nchini humo. huku Baadhi ya Wakongomani wanahoji kuhusu hatua ya Rais Tshisekedi kutaka kuibadili Katiba.

Tangu miongo kadhaa iliyopita, Katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo haijawaruhusu Wakongomani kushikilia uraia mwengine.

Suala hilo limewasilishwa mezani zaidi ya mara moja chini ya utawala wa rais wa zamani Joseph Kabila, haswa ili kutaka kuwaruhusu Wakongomani walio ughaibuni kushiriki katika uchaguzi, lakini hili halijawahi kufanikiwa.

Jumamosi iliyopita, wakati wa mkutano ambapo Rais Tshisekedi aliwataka wabunge walio upande wake kuipitisha serikali ya Waziri Mkuu Sama Lukonde, rais alisisitiza kujitolea kwake ili kusuluhisha suala hilo la uraia wa nchi mbili.

''Tumefanya kampeni nje ya nchi na Wakongomani ambao wana uraia mwengine na ambao wanapigania Kongo sawa na wale walio hapa nchini. Sioni haki kuendelea kuwaweka kando. Lazima tuwaruhusu wenzetu walioko ughaibuni kuweza kuwa na raha.''

Wabunge zaidi ya 350 walishiriki mkutano huo ambao Tshisekedi aliyagusia pia masuala mengine ambayo yanahitaji suluhisho la haraka, yakiwemo na usalama kwenye eneo la mashariki.

Raia wa Congo wanahoji sababu hasa ya Tshisekedi kulivalia njuga suala hilo

Lakini kuhusu swali hili la uraia wa nchi mbili, Wakongomani wengi wanahoji masuala kadhaa kuhusu sababu halisi ya mradi huo, ikiwa sio kufikia sheria itakayotengenezwa kwa faida ya mtu binafsi, familia au kikundi cha watu.

soma zaidi: Hali ya wasiwasi mashariki mwa DRC kufuatia mashambulizi

Moja wa Wakongomani hao ni Profesa Mushi Bonane kutoka Chuo Kikuu cha Kiprotestanti nchini Kongo (UPC).

''Ndiyo ni swali la muhimu, lakini sheria yoyote inayochukuliwa kwa ajili ya shida za mtu moja au za kikundi cha watu, hiyo hatua haipaswi kuambatana na katiba ya nchi. Sheria inapaswa kuchukuliwa kwa kumaliza shida ya raia kwa wingi. Nahisi ndugu rais anaenda mbio sana.''

Rais Tshisekedi mwenyewe ana uraia mwengine. Kinachowagusa sana Wakongomani siku hizi ni hali ya ukosefu wa usalama mashariki mwa nchi hii. Wengi wanawaza hicho ndicho kipaumbele cha juu.

Mwandishi:  Jean Noel Ba-Mweze, DW, Kinshasa.