1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump awatembelea wanajeshi wa Marekani nchini Iraq

27 Desemba 2018

Rais wa Marekani Donald Trump amefanya ziara ya Iraq – ambayo ni yake ya kwanza kuwatembelea wanajeshi wa Marekani katika eneo la kivita tangu alipochaguliwa

https://p.dw.com/p/3AfmP
Trump besucht US-Truppen im Irak
Picha: Reuters/J. Ernst

Rais Trump ameitumia ziara yake ya Iraq kutetea uamuzi wake wa kuwaondoa wanajeshi wa Marekani nchini Syria na kutangaza kuwa jukumu la Marekani sio kuwa "polisi” ya ulimwengu. 

Trump alitua katika Kituo cha Jeshi la Anga cha Al-Asad magharibi mwa Iraq, saa moja na dakika 16 za jioni saa za nchini humo, akiandamana na mkewe Melania, kufuatia kile alichokieleza kuwa ni safari ngumu na yenye usiri mkubwa kwenye ndege ya Air Force One ambayo ilizimwa taa zote.

Rais huyo alikihutubia kikundi cha karibu maafisa 100 wengi wao wa vikosi maalum na kisha viongozi wa kijeshi kabla ya kuondoka masaa machache baadaye. Mkutano uliopangwa na Waziri Mkuu wa Iraq Adel Abdel-Mahdi ulifutwa na badala yake viongozi hao wawili wakazungumza tu kwa njia ya simu. Msemaji wa Ikulu ya White House Sarah Sanders amesema kuwa wakati mazungumzo hayo Trump alimualika Abdel Mahdi kuzuru Washington na akakubali.

Trump besucht US-Truppen im Irak
Trump aliandamana na mkewe MelaniaPicha: Reuters/J. Ernst

Ziara za kutia moyo za marais kuwatembelea wanajeshi wa Marekani katika maeneo ya kivita zimekuwa utamaduni wa muda mrefu katika miaka iliyofuata mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, 2001.

Akizungumza katika kituo cha kijeshi nchini Iraq, Trump aliitetea sera yake ya "Marekani Kwanza” ya kujiondoa kutoka miungano ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na kile kwa Wamarekani wengi kinaonekana kuwa ni vita visivyokuwa na kikomo katika Mashariki ya Kati "Marekani haipaswi kuwa inapigana kwa niaba ya kila taifa duniani. Kama wanataka tupigane kwa niaba yao, wanapaswa pia kulipia gharama na hivyo wakati mwingine inahusu gharama ya kifedha".

Trump amewaambia wanahabari kuwa aliwapinga majenerali waliomtaka arefushe muda wa jeshi la Marekani nchini Syria, ambako karibu askari 2,000, wakishirikiana na wanajeshi wengine wa kigeni, wanawasaidia wapiganaji wa nchini humo kupambana na kundi la jihadi linalojiita Dola la Kiislamu – IS. Trump amesema kuwa wamefanikiwa kulitokomeza kundi hilo ambalo wakati mmoja liliyadhibiti maeneo ya mipaka ya Iarq na Syria.

Nchini Afghanistan, Trump anataka kuondoa karibu nusu ya wanajeshi 14,000 wanaopambana na wanamgambo wa Taliban. Baada ya kuondoka Iraq, Rais huyo wa Marekani alipitia katika Kituo cha Jeshi la Anga cha Ramstein nchini Ujerumani, ambako yeye na Melania walikutana na kuwasalimia baadhi ya mamia ya wanajeshi waliokusanyika. Rais na ujumbe wake kisha wakaelekea Marekani.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Grace Patricia Kabogo