Tetemeko jingine latokea Chile | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 01.03.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Tetemeko jingine latokea Chile

Tetemeko la ardhi lenye kipimo cha richta 6.2 limetokea usiku wa jana siku moja baada ya kutokea tetemeko jingine lililokuwa na kipimo cha richta 8.8

default

Mwanamke akiangalia majengo yaliyoanguka huko Talcahuano, Chile, kufuatia tetemeko la ardhi lililoikumba nchi hiyo siku ya Jumamosi.

Tetemeko jingine la ardhi lenye kipimo cha richta 6.2 limetokea kati kati mwa Chile usiku wa jana, siku moja baada ya kutokea tetemeko jingine la ardhi lililokuwa na kipimo cha richta 8.8 na kusababisha vifo vya watu 700. Taasisi ya Ukaguzi wa Jiologia nchini Marekani, imesema kitovu cha tetemeko hilo la ardhi kilikuwa kilometa 35 chini ya bahari na umbali kilometa 160 kaskazini-mashariki mwa mji wa Talca.

Kufuatia matetemeko hayo ya ardhi, serikali ya Chile imeomba radhi kwa kushindwa kutoa onyo la kutokea mawimbi ya tsunami kutokana na tetemeko la ardhi la siku ya Jumamosi, lililosababisha vifo vingi katika eneo la pwani mwa nchi hiyo. Aidha, serikali ya nchi hiyo imetangaza amri ya kutotembea katika maeneo mawili yaliyoathiriwa zaidi na tetemeko hilo la ardhi, katika mkoa wa Maule na mji mkuu wa pili wa Concepcion pamoja na majimbo yake, ambako wasi wasi wa hali ya usalama umeongezeka kufuatia polisi kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya baadhi ya watu waliokuwa wakipora katika maduka.

Idadi ya waliokufa huenda ikaongezeka

Rais Michelle Bachelet wa Chile amesema anatarajia idadi ya waliouawa na tetemeko hilo la ardhi ikaongezeka na kufikia 708, huku serikali yake ikikiri kushindwa kutoa onyo kwa wananchi kuhusu hatari ya kutokea mawimbi ya tsunami. Meya wa mji wa Concepcion, Jacqueline van Rysselberghe ameomba msaada wa dharura wakati waokozi wakiendelea na zoezi la kuwatafuta watu waliokwama katika majengo yaliyoanguka, hasa katika mji huo.

Rais Bachelet anayetarajiwa kukabidhi madaraka kwa mrithi wake, Sebastian Pinera tarehe 11 ya mwezi huu, amesema vikosi vya jeshi la anga vitaanza kugawa chakula na mahitaji muhimu katika maeneo yaliyoathiriwa vibaya na tetemeko hilo la ardhi. Kiasi watu milioni mbili wameathiriwa na tetemeko hilo la ardhi. Televisheni ya taifa imetangaza kuwa maiti 300 zimepatikana hadi sasa. Tetemeko hilo la ardhi ambalo ni kubwa na baya zaidi kuwahi kutokea nchini humo tangu miaka 50 limeteketeza nyumba milioni 1.5. Kituo cha kihistoria cha mji wa Curico kimeharibiwa kwa asilimia 90 na tetemeko la ardhi. Rais Barack Obama wa Marekani ametoa salamu za pole kwa Rais Bachelet na kuelezea nia yake ya kuisaidia nchi hiyo. Rais Obama alisema,''Marekani iko tayari kusaidia katika jitihada za uokozi na tuna vifaa kwa ajili ya uokozi kama serikali ya Chile itaomba msaada wetu. Chile ni rafiki na mshirika wa karibu wa Marekani na nimemfahamisha Rais Bachelet tupo kwa ajili yake endapo wananchi wa Chile watahitaji msaada wetu.''

Kitovu cha tetemeko hilo la ardhi kilikuwa maili chache kaskazini mwa tetemeko kubwa la ardhi kuwahi kurekodiwa la Mei, mwaka 1960 lililokuwa na kipimo cha richta 9.5 ambalo lilisababisha vifo vya kati ya watu 2,200 na 5,700. Nchi za eneo la Pacific na mataifa yote 53, katika eneo la pwani ya Magharibi ya Kusini na Amerika ya Kati, yameondoa onyo la kutokea kwa tsunami. Ukilinganisha na tetemeko lililotokea Haiti mwezi Januari lililokuwa kipimo cha richta 7.0, watu 217,000 waliuawa.

Clinton kuzuru Santiago

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton, aliyepanga kufanya ziara Amerika ya Kusini kabla ya kutokea janga hilo, kesho Jumanne atazuru Santiago na anatarajiwa kukutana na Rais Bachelet na Pinera. China kwa upande wake imesema itachangia dola milioni moja kwa ajili ya kusaidia juhudi za dharura za kibinaadamu nchini Chile.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)

Mhariri: Mwadzaya,Thelma

 • Tarehe 01.03.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/MEjG
 • Tarehe 01.03.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/MEjG
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com