Taswira baada ya mlipuko wa Beirut — uharibifu, taharuki na juhudi za uokozi
Mlipuko mkubwa umeukumba mji mkuu wa Lebanon, Beirut na kuua watu wasiopungua 100 na kujeruhi maelfu wengine. Hospitali zimezidiwa na kuomba msaada wa haraka wa kupatiwa damu.
Taharuki mjini Beirut
Milipuko miwili mikubwa yaitikisa Beirut na maeneo jirani ya mji huo mkuu wa Lebanon na kuzusha taharuki huku wakaazi wake wakikimbia hovyo kutafuta hifadhi. "Kwenye maisha yangu sijawahi kuona janga kubwa kama hili," Gavana wa mji wa Beirut alikiambia kituo kimoja cha televisheni.
Kishindo cha milipuko kilifika hadi maeneo ya pembezoni ya mji huo
Mtikisiko wa milipuko hiyo, iliyotokea katika eneo la bandari ya Beirut ulifika kila kona ya mji huo mkuu. Hata wakaazi wa maeneo ya pembezoni waliripoti kusikia kishindo chake, huku wengine wakisema madirisha yao ya vioo yalivunjika.
Mamia wamepoteza maisha, maelfu wengine wamejeruhiwa
Wizara ya afya ya Lebanon imesema zaidi ya watu 100 wamekufa na zaidi ya wengine 4,000 wamejeruhiwa.
Shehena hatari ya kemikali ya ammonium nitrate
Waziri Mkuu Hassan Diab alisema shehena kubwa ya tani 2,750 ya kemikali hatari ya ammonium nitrate iliyohifadhiwa katika ghala moja kwenye bandari ndiyo ilisababisha mlipuko mkubwa wa pili. "Hii haikubaliki kwamba tani 2,750 za ammonium nitrate zimehifadhiwa hapa kwa miaka sita bila kuchukua hatua zozote za tahadhari," alisema Diab.
Juhudi za kunusuru majeruhi
Zaidi ya vikosi 30 vya Shirika la Msalaba Mwekundu vilikwenda kwenye eneo la tukio huku wakishirikiana na wakaazi wa mji huo kutoa msaada katika juhudi za uokozi. Hospitali ziliarifu mara moja kuwa zimeanza kuzidiwa - na kutoa wito wa kuchangiwa damu pamoja na majenereta ya kuhakikisha kunakuwa na umeme.
Kishindo cha milipuko kilisikika hadi Cyprus
Kulingana na kituo cha sayansi ya miamba cha Ujerumani milipuko hiyo ilisababisha tetemeko la ukubwa wa 3.5 katika kipimo cha matetemeko ya ardhi. Wakaazi wa Cyprus, kiasi kilometa 180 kutoka Beirut waliarifu kuwa walisikia kishindo chake.
Hamkani ya kutafuta ndugu na jamaa
Mwandishi wa DW, Bassel Aridi alisema, watu walikwua wakitumia mitandao ya kijamii kuwatafuta wapendwa wao baada ya milipuko. Aridi pia alitembelea hospitali mjini Beirut baada milipuko. "Kile nilichokiona hospitali kilikuwa cha kutatiza. Hospitali zote ziliripoti kuwa zimezidiwa wagonjwa"
Hali ya dharura yatangazwa kwa wiki mbili
Mamlaka za Lebanon zinahofia kuwa watu wengi bado wamefukiwa chini ya vifusi. Na rais Michel Auon alifanya mkutano wa Baraza la Mawaziri siku ya Jumatano na kutangaza hali ya dharura ya wiki mbili.
Lebanon yakabiliwa na majanga mawili
Milipuko mjini Beirut imetokea wakati Lebanon inapitia kipindi kigumu cha hali dhaifu ya uchumi huku mamia ya watu wakiingia mitaani kuandamana dhidi ya hali mbaya ya kifedha. Waziri Mkuu Hassan Diab alitangaza siku ya Jumatano ya August, 5 kuwa siku ya maombolezo ya taifa.