1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yawaondoa Wamaasai katika maeneo ya utalii

9 Julai 2024

Serikali ya Tanzania inafanya upanuzi wa hifadhi zake za asili kwa kuwaondoa wafugaji wa jamii ya Kimasai waliokuwa wanaishi katika maeneo hayo tangu enzi. Mpango huo unalenga kuvutia utalii wa kifahari zaidi.

https://p.dw.com/p/4i4JZ
Tanzania, Ngorongoro | Masai
Baadhi ya Wamasai wakiwa kwenye mkutano kujadili mgogoro wa ardhi baina yao na serikali.Picha: Deinis Olushangai

Maisha yanazidi kuwa magumu kwa kabila la Wamasai wa Tanzania. Mwakilishi wa kundi la wanawake wa kimasai ambaye hakutaka jina lake liwekwe wazi  kutokana na usalama wake ameiambia DW kwamba wawakilishi wengi wa wafugaji wa kabila hilo wamekamatwa katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita kila walipokosoa sera hizo za upanuzi wa maeneo hayo zinazotekelezwa na serikali ya Tanzania.

Nikinukuu maneno yake mwakilishi huyo anasema "wanawake wawili wajawazito walipoteza maisha hivi majuzi kutokana ana mvua kubwa na ubovu wa barabara."

Mwanamke huyo aliongeza kuwa karibu kila wiki kuna mjamzito anafariki dunia katika Hifadhi ya Ngorongoro na Loliondo na kwamba serikali ya Tanzania ndiyo inayopaswa kulaumiwa.

Huduma za kuwasafirisha wagonjwa katika maeneo hayo zimesimama katika kile kinachotajwa kuwa ni namna ya kuishinikiza jamii hiyo ya wamasai kuhama katika maeneo hayo.

Kwa upande wake msemaji mkuu wa serikali ya Tanzania alipotafutwa kutoa ufafanuzi kuhusu hilo na DW hakutoa ushirikiano juu ongezeko la ubovu wa huduma za kiafya katika maeneo hayo.

Soma pia:HRW: Kufukuzwa kwa Wamasai huko Loliondo kumekiuka haki zao

Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inayo mipnago ya kupanua  maeneo ya uhifadhi kutoka 30% hadi 50%  nchini Tanzania.

Hata hivyo mpango wa serikali hiyo ya Tanzania unaonekana kupokelewa kwa maoni mseto. Sheria za uhifadhi zinaeleza kwamba hakuna watu anayetakiwa kukaa katika maeneo hayo na kwamba hakuna makazi, wala shule ama hospitali ambazo zinaweza kujengwa katika maeneo hayo.

Joseph Oleshangay, Chifu wa wamasai Ngorongoro aliiambia DW kwamba kuna ubaguzi wa ujenzi wa miundombinu hasa katika jamii zinazokaa katika maeneo hayo.

Kiongozi huyo wa wamasai aliongeza kuwa Aprili 12, 2021, serikali ya Tanzania ilitoa taarifa kwa umma kutangaza nia yake ya kubomoa shule tisa za serikali, vituo vya afya sita, vijiji tisa na makanisa manne, na baada ya hapo aliwasilisha malalamiko mahakamani na mahakama iliiamuru serikali kusitisha mpango huo.

Chini ya mpango huo Tanzania itaongeza pato lake?

Mpango wa Tanzania wa kupanua maeneo ya hifadhi unatarajiwa kuvutia mabilioni ya uwekezaji kutoka nje pamoja na watalii zaidi. Mwaka uliopita, zaidi ya watu milioni moja walitembelea mbuga za wanyama za Tanzania.

Baadhi ya wamasai Tanzania waandamana kupinga kuondoshwa eneo la hifadhi

China, kwa mfano, iliwekeza zaidi ya dola milioni 9 katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, iliyopewa jina la Bonde la Ngorongoro. Eneo hilo lilikuwa na uzio ili kulinda kambi za watalii, hoteli za kifahari na maeneo ya kifahari ambayo awali yalikaliwa na Wamasai.

Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) nao umewekeza zaidi ya dola bilioni 7 nchini Tanzania. Miongoni mwa eneo la uwekezaji wao ni neo la uwindaji huko Loliondo.

Nyumba za kulala wageni za kifahari na uwanja wa ndege kwa ajili ya ndege za kibinafsi vinajengwa ili kuwakaribisha watalii watakaofika kwa shughuli za uwindaji.

Soma pia:Kupotea kwa Serengeti - Ardhi ya Wamaasai

Bunge la Tanzania kwa sasa linajadili pendekezo lingine ambapo mpango uliopo utahitaji kuondolewa kwa angalau vijiji 100 zaidi vya Wamasai sawa na kusema ya zaidi ya watu 300,000 watalazimika kuyahama makazi yao.

Ikiwa mipango hiyo itatekelezwa, Wamasai watapoteza 80-90% ya ardhi yao ya asili na hiyo ni kwa mujibu shirika lisilo la kiserikali la Roman Herre la hapa Ujerumani ambalo linaunga mkono haki za Wamasai.

Itakumbukwa kuwa mwezi Aprili mwaka huu,  Benki ya Dunia ilisitisha ufadhili wa upanuzi wa maeneo ya utalii wa Euro milioni 150 kwa Tanzania kutokana na masuala ya haki za binadamu. Na mnamo Juni, Halmashauri Kuu ya Ulaya pia iliondoa zabuni ya mradi yenye thamani ya Euro milioni 10.