1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yatafuta uponyaji baada ya vurugu za Uchaguzi Mkuu

11 Novemba 2025

Siku chache baada ya vurugu uchaguzi Mkuu wa Tanzania, Oktoba 29 kumekuwa na majeraha, kiwewe na athari za kisaikolojia kwa Watoto. Wakiwa wameathirika na milio ya risasi na mabomu, Je watoto hawa wanasaidiwa vipi?

https://p.dw.com/p/53Q2s
Tanzania Dar es Salaam 2025 | Waandamanaji wakipambana na vikosi vya usalama
Vikosi vya usalama vikipambana na waandamanaji waliojitokeza Jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, Oktoba 29, 2025Picha: Onsase Ochando/REUTERS

Ni dhahiri kuwa macho ya watoto yaliona zaidi ya kile ambacho macho yao yanavyoweza kustahimili. Walishuhudia ndugu wakijeruhiwa, walisikia milio ya risasi, mabomu ya machozi na keleleza waandamanaji. Kwa umri wao hizi ni kumbukumbu zinazoweza kubaki kwa muda mrefu.

Vurugu za Oktoba 29 hazikuacha makovu kwa wanaume na wanawake tu bali hata kwa Watoto.Ambao wamekuwa na maswali lukuki juu ya nini kilichosababisha, na nini kitafuata.

"Watoto wana hofu kubwa"

Joyna Mapungu, ni mzazi na mkazi wa Kimara, Dar es Salaam "Kwa kweli watoto walikuwa na hofu kubwa hata ukitaka kutoka watoto wanapiga kelele. Halafu kuna kitu kingine mimi kilinishangaza siku moja mtoto wangu alitoka nje na hakuona mtu yoyote akarudi ndani mbio akiwa na hofu akauliza mama watu wameenda wapi,?"

Tanzania Dar es Salaam 2025 | Waandamanaji wakati wa Uchaguzi Mkuu Jijini Dar es Salaam
Moshi ukionekana katika eneo moja jijini Dar es Salaam, Tanzania. Kuliibuka maandamano yaliyogubikwa na vurugu jijini humo katika siku ya uchaguzi, Oktoba 29, 2025Picha: AFP

Wataalamu wa afya ya akili wanasema matukio kama haya yanaweza kusababisha kiwewe cha kisaikolojia kwa watoto.Wengine wanaanza kujitenga na wenzao, wengine hukataa kwenda shule au kushindwa kuzungumza kabisa, kama mwanasaikolojia Saldine Kimangale anavyosema. "Watoto huwa wana'react' tofauti kwa sababu wao hawana njia sahihi ya kueleza hisia zao.. kwa hiyo mara nyingi unaweza kuona wao wanakuwa na mabadiliko ya tabia ambayo hayakutarajiwa. Kwa mfano unaweza kuona mtoto labda ameanzisha tabia ya kulialia..."

Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 uligubikwa na vurugu za maandamano ya vijana waliokuwa wakidai haki. Vurugu hizo ziliviinua vyombo vya ulinzi na usalama ambao walichukua hatua na kusababisha kuwepo kwa milio ya risasi, mabomu na mauaji ya watu.

Watahiniwa wapewa fursa maalumu ya kuikabili hofu na wasiwasi

Haya yote yanajiri wakati ambapo wanafunzi wa kidato cha pili wanatarajia kuanza mitihani yao ya taifa, Jumatatu Novemba 10 badala ya Novemba 3, na Kidato cha nne wakitarajiwa kuanza mitihani yao Novemba 24 badala ya Novemba 17.

Hotuba ya Samia baada ya kuapishwa

Ili kuweka hali hasa kwa watahiniwa, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya  Mugabe jijini Dar es Salaam amesema imewalazimu kuzungumza na watahiniwa ili kuwatoa kwenye athari za kisaikolojia kabla ya mitihani. Mwalimu Mathewe Mchome alipozungumza na DW alisema "Tumetengeneza timu ya walimu ambao sisi tunaamini kwa uelewa wao wanaweza kutambua watoto wanaoonekana kuwa na msongo wa mawazo kidogo." Akaongeza kuwa wanaangalia namna ya kuingiza masuala ya amani kwenye baadhi ya masomo.

Mashirika ya kiraia yanatoa wito kwa serikali na wadau wa maendeleo kuweka mipango ya ushauri nasaha, hasa kwa watoto waliokuwa mashuhuda wa vurugu hizo. Kwao, si tu matukio ya kisiasa—ni ndoto mbaya zinazoweza kuendelea hata baada ya nchi kurudi katika utulivu.

Wataalamu wanasema, kuponya makovu ya risasi ni rahisi kuliko kuponya makovu ya nafsi. Watoto hawa wanahitaji zaidi ya ukimya na muda, wanahitaji kusikilizwa, kuhurumiwa na kusaidiwa kurejea katika hali yao ya kawaida.