1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yalaani mapigano yanayoendelea Sudan

19 Aprili 2023

Serikali ya Tanzania imesema ikiwa kama mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika inalaani vikali mapigano yanayoendelea Sudan na kuzitaka pande zinazozozana kuacha mapigano mara moja.

https://p.dw.com/p/4QHmd
Sudan | Kämpfe in Khartum
Kumekuwa na uharibifu na hasara KhartoumPicha: REUTERS

Aidha, imewataka pia raia wake walioko nchini humo kuchukua tahadhari wakati serikali ikitafakari juu ya mustakabali wao. 

Soma pia: Sudan: Kuna kauli zinazokinzana juu ya usitishaji mapigano

Ikiungana na mataifa mengine kutoa wito wa kusitishwa kwa mapigano yanayoshuhudiwa katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, Tanzania imesema mizozo ya kivita ni mwiba unaozichoma na kuzisambaratisha familia na kwa maana hiyo kuegemea mapigano kama shabaha ya kufikia azma ya kisiasa haiwezi kukubalika katika jumuia ya kimataifa.

Imezitolea mwito pande zinazohasimiana katika uwanja huo wa vita kujizuia na matumizi yoyote ya nguvu na kuacha mkondo wa majadiliano kuchukua nafasi.

Stergomena Tax SADC
Waziri Stergomena Tax asema Tanzania inafuatilia hali SudanPicha: Valery Sharifulin/TAS/dpa/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje, Stergomena Tax amesema uwanja wa mapambano umezidisha hali ya wasiwasi kwa shughuli za kibinadamu, hatua ambayo inaongeza kitisho kwa raia wanaoathiriwa na mapigano hayo.

Mapambano ya kuwania madarakani nchini Sudan yamekuwa kiini cha mzozo unaoyagharimu maisha ya mamia ya raia, huku jumuiya ya kimataifa ikiendelea kutoa mwito wa kusitisha mapigano hayo yaliyozuka tangu Jumamosi iliyopita.

Wakati huo huo, Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye makao yake makuu mjini Arusha, Tanzania, imehimiza kufanyika kwa mazungumzo ili kuumaliza mkwamo huo na kuzitaka pande zinazokwaruzana kutumia jumuiya za kikanda kama njia muafaka itakayoweza kutuliza hali ya mambo.

Ama kuhusu raia wa Tanzania walioko nchini Sudan, Waziri Stergomena amesema serikali inaendelea kuufatilia kwa karibu mzozo huo lakini imeashiria uwezekano wa kuanza kuwaondoa iwapo mapigano hayo yataendelea.

Baadhi ya nchi za Afrika Mashariki zimeashiria uwepo wa maandalizi ya kuwaondoa raia wake ikiwamo nchi jirani ya Kenya.

Hata hivyo, haijafahamika namna nchi hizo zitakavyofaulu kuwasafirisha raia hao hasa kutokana na huduma nyingi kusimama ikiwamo uwanja wa ndege wa Khartoum uliofungwa tangu yalipozuka mapigano hayo.