1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroNigeria

Taarifa mbaya zinaathiri vita dhidi ya utekaji nyara Nigeria

26 Machi 2024

Mkuu wa majeshi wa Nigeria Chris Musa amesema jeshi linapewa taarifa mbaya za kijasusi na watoa habari jambo linalotatiza vita dhidi ya magenge yenye silaha yanayohusika na visa vya utekaji nyara.

https://p.dw.com/p/4e75o
Wanafunzi wa shule waliotekwa Kaduna
Jeshi la Nigeria liliwaokoa wanafunzi zaidi ya 130 wa shule waliotekwa na watu wenye silaha KadunaPicha: Ibrahim Yakubu/DW

Mkuu wa majeshi wa Nigeria Chris Musa amesema jeshi linapewa taarifa mbaya za kijasusi na watoa habari jambo linalotatiza vita dhidi ya magenge yenye silaha yanayohusika na visa vya utekaji nyara na ambayo yanaendelea kuwateka wanafunzi na wakazi kaskazini mwa nchi hiyo. Jeshi lilitangaza kuwa liliwaokoa wanafunzi 137 waliotekwa na watu wenye silaha mapema mwezi huu kaskazini magharibi mwa jimbo la Kaduna.

Watoto hao wa shule waliwasili Kaduna jana tayari kuunganishwa na familia zao. Musa ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa jeshi linapitia changamoto nyingi na aghalabu huwategemea watoa taarifa ili kuyasaka magenge yenye silaha, na mara nyingi bila kufua dafu. Amesema watoa taarifa huwafanya wanajeshi kwenda kwingine na wakati wanapofika huko, hawakuti chochote na kuwaruhusu magenge hayo kufanya vitendo vya uhalifu.

Soma pia: Watekaji hawajalipwa kikomboleo kama walivyodai

Musa amesema hakukuwa na makabiliano kati ya jeshi na watekaji wakati wa kuwaokoa wanafunzi hao wa Kaduna. Lakini hakusema ni jinsi gani wanafunzi hao waliachiliwa huru au kama mshukiwa yeyote wa utekaji huo alikamatwa.