Syria yakanusha madai ya kushambuliwa msafara wa Assad | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.08.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Syria yakanusha madai ya kushambuliwa msafara wa Assad

Huku waasi nchini Syria wakidai kuushambulia msafara wa magari ya Rais Bashar Al Assad hii leo asubuhi, serikali ya nchi hiyo imekana madai hayo ikisema hayana ukweli wowote.

Waziri wa habari nchini Syria Omran al-Zohbi

Waziri wa habari nchini Syria Omran al-Zohbi

Serikali ya Syria imekanusha vikali ripoti kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini humo kwamba msafara wa Rais Assad umeshambuliwa leo asubuhi.

Vyombo tofauti vya habari ikiwemo televisheni ya Al Arabiya vimeripoti kutokea kwa mashambulizi ya roketi yaliyoulenga msafara wa Rais Assad.

Wakati wa mashambulizi hayo Rais Assad alikuwa akielekea katika msikiti wa Anas bin Malik ulioko katikati mwa mji wa Damascus kuhudhuria sala ya Idd ul Fitr inayoadhimisha kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Rais Assad akisali Sala ya Idd ul Fitr

Rais Assad akisali Sala ya Idd ul Fitr

Kulingana na waziri wa habari nchini humo, Omran al-Zohbi, taarifa za mashambulizi hayo hazina ukweli wowote.

Waziri Zohbi amesema Rais Assad aliokuwa akiendesha gari lake mwenyewe, alihudhuria sala hiyo na pia kusalimiana na waumini wengine waliokuwa msikitini.

Kwa upande wake shirika la kutetea haki za binaadamu la Syria lililo na makao yake mjini London limesema haliwezi moja kwa moja kuthibitisha mashambulizi hayo lakini hii leo asubuhi mashambulizi ya roketi yalikumba eneo la Malki mahali ambapo Rais Assad alihudhuria sala yake ya Idd Ul Fitr.

Assad alionekana katika televisheni ya kitaifa akikaa pamoja na wajumbe wengine akiwa mtulivu huku akitabasamu katika sala hiyo ya Iddi hii leo asubuhi.

Katika maombi yake Imamu wa msikiti huo Ahmed al-Jazairi, aliomba akisema kwamba "Ewe Mwenyezi Mungu mpe Rais Assad mafanikio kwa ajili ya mustakbal wa nchi ya Syria".

Shambulizi la waasi

Shambulizi la waasi

Waasi wakiri kuhusika na shambulizi

Hata hivyo, pamoja na serikali kukana madai ya kushambuliwa kwa msafara huo, upinzani umedai kuhusika na mashambulizi hayo leo asubuhi. Firas al-Bitar, kiongozi wa kundi la upinzani la Ahrar al-Sham aliviambia vyombo vya habari kuwa wapiganaji wa jeshi lake waliushambulia msafara wa Assad.

Hapo jana vikosi vya serikali ya Assad viliwashambulia waasi kaskazini Mashariki mwa Damascus na kusababisha mauaji ya wapiganaji 60 wa waasi.

Ni nadra sana kwa Rais Assad kuonekana hadharani tangu kuanza kwa machafuko nchini Syria mwaka wa 2011 ambapo zaidi ya watu 100,000 wameuwawa na wengine wengi kupoteza makaazi yao.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/AP/Reuters/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com