Syria tayari kwa mazungumzo | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.01.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Syria

Syria tayari kwa mazungumzo

Rais wa Syria, Bashar al-Assad amesema serikali yake iko tayari kujadiliana mapendekezo ya mazungumzo ya amani yaliyopangwa kufanyika nchini Kasakhstan,

Tarehe rasmi ya kufanyika kwa mazungumzo hayo bado haijapangwa rasmi, pamoja na mwakilishi wa upinzani kwenye mazungumzo hayo pia hajatajwa.

Rais Bashar al-Assad aidha amesema, mpango wa kusitisha mapigano uliofikiwa chini ya Urusi na Uturuki ambao ni washirika wake wakubwa, ulivunjwa na majeshi, na sasa yataikamata Syria, ikiwa ni pamoja na maeneo yaliyokuwa yakikaliwa na waasi yaliyopo karibu na mji wa Damascus, ambako chanzo kikuu cha maji kiliharibiwa na mabomu.  

Ametoa matamshi hayo alipokuwa akitoa maoni yake wakati akizungumza na kituo cha  habari cha Ufaransa, ambayo yalirushwa na taasisi ya habari ya serikali nchini Syria, SANA.

Mwezi uliopita, Urusi ilisema imefikia makubaliano na Assad, Iran na Uturuki kwamba mji wa Kazakhstan ulioko Astana ndi utakuwa eneo litakalotumika kwa mazungumzo hayo mapya ya amani baada ya waasi kuangushwa vibaya katika vita vya kuwafurusha eneo la Mashariki mwa Syria, Aleppo. 

Urusi na Uturuki ambao ni wafadhili wakuu katika mapambano dhidi ya upinzani unaompinga Assad, wamekubaliana kuleta suluhu kama hatua muhimu ya kurejesha diplomasia, ingawa pande zinazokinzana zimeendelea kushutumiana kwa ukiukwaji wa mara kwa mara wa hatua kama hizo.   

Assad amesema wawakilishi wa serikali wapo tayari kwenda Astana, wakati muda wa mazungumzo utakapopangwa. 

Awali, Rais Assad aliutetea uamuzi wa majeshi ya serikali kufanya mashambulizi makali ya katika mji wa Aleppo na kuukomboa mji huo kutoka kwa waasi mnamo wiki tatu zilizopita. Amesema njia mbadala ilikuwa ni kuwaacha raia kuendelea kusalia mji huo na kusubiri huruma ya magaidi, neno ambalo serikali imekuwa ikilitumia kwa yoyote anaepingana na utawala wa Assad.

Katika hatua nyingine, waziri wa masuala ya kigeni wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema anataraji Marekani itamrejesha kiongozi wa kidini aliyehusishwa na kuandaa mapinduzi yaliyofeli nchini Uturuki mwezi Julai mwaka jana, anayeishi uhamishoni nchini humo lakini pia akitaka Marekani kusitisha mahusiano na kundi la wapiganaji la YPG nchini Syria. 

Mwandishi: Lilian Mtono.
Mhariri: Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com