Syria kutangaza kuacha mapigano
25 Oktoba 2012Kundi la waasi linalojita Jeshi Huru la Syria (FSA) limehakikisha kuacha mapigano katika kipindi cha siku nne za maadhimisho ya sikukuu ya Eid al-Hajj inayoanza kesho lakini kwa masharti watatekeleza hatua hiyo, ikiwa tu upande wa serikali nao utaheshimu kwa dhati makubaliano hayo.
Msemaji wa FSA, Kanali Kassim Saad Eddine, amesema watafuatilia kwa umakini endapo majeshi ya serikali yatakuwa yanatekeleza hatua hiyo. Hata hivyo, kikundi kingine cha waasi kiitwacho al-Nusra Front, kimekwisha litupilia mbali pendekezo la Brahimi la kuacha mapigano.
Taarifa za hivi punde, kwa mujibu wa Shirika la Uangalizi wa Haki za Binadamu la Syria, zinaeleza kwamba majeshi ya serikali yameshambulia makazi ya waasi katika viunga vya jiji la Damascus na watu watano kuuwawa. Shirika hilo lenye makao yake makuu mjini London, nchini Uingereza, limesema pia kiasi ya watu 220 waliuwawa jana katika mapigano yaliyotokea katika maeno tofauti nchini Syria.
Uchunguzi wa vitendo vya uhalifu
Katika hatua nyingine jopo huru linalofanya uchunguzi kuhusu tuhuma za vitendo vya uhalifu wa kivita nchini Syria linahitaji mkutano wa haraka iwezekanavyo baina yake na Rais Bashar al Assad. Mkuu wa jopo hilo mwanadiplomasia Sergia Pinheiro, amesema jopo lake linaomba kukutana na kiongozi huyo bila masharti yoyote.
Chombo cha juu kabisa cha haki za binadamu cha Umoja wa Mataifa kilimtaka Pinheiro sambamba na wanachama wengine watatu katika jopo hilo akiwemo mwendesha mashitaka wa zamani wa uhalifu wa kivita anaeheshimika wa Umoja wa Mataifa, Carla Del Ponte, kuendelea na uchunguzi wao hadi Machi mwakani.
Del Ponte, ambaye pia ni mwanasheria mkuu wa zamani wa serikali ya Uswisi, amesema uchanguzi wao kwa hivi sasa unatafuta washukiwa wa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita katika kipindi hiki ambacho machafuko ya umwagikaji damu yamezidi kuongezeka nchini Syria.
Duru nyingine zinasema Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Hillary Clinton amesema kuna hatari Syria inaweza kujaza ombwe la kisiasa nchini Lebanon, na hivyo amewataka wanaisiasa wa taifa hilo kuunda serikali isio na shinikizo lolote kutoka nje. Waziri huyo wa mashauri ya kigeni amesema Marekani inamuunga mkono Rais Michel Suleiman wa Lebanon katika kuunda serikali mpya baada ya mauwaji ya afisa wa juu kabisa wa usalama wa taifa hilo, katika mripuko uliyotokea katika gari Oktoba 19.
Mwandishi: Sudi Mnette/APE/DPA
Mhariri: Mohammed Khelef