Ngoma nzito kambi ya Wad al-Daif Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.10.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ngoma nzito kambi ya Wad al-Daif Syria

Waasi nchini Syria wanaendelea na mapambano kuiteka kambi ya kijeshi ya Wadi al-Daif iliyoko karibu na njia kuu ya kutoka kaskazini kuelekea kusini ambayo ni muhimu kwa waasi hao kudhibiti kabisaa sehemu ya kaskazini

Ndege ya jeshi la Syria ikiwa katika anga ya mji wa Aleppo.

Ndege ya jeshi la Syria ikiwa katika anga ya mji wa Aleppo.

Kwa muda wa wiki mbili waasi wameizingira na kuishambulia kambi ya Wadi al-Daif lililoko mashariki mwa mji wa Maaret al-Numan. Wanasema ukali wa mashambulizi kutoka kwa vikosi vya serikali unaonyesha ni kwa kiasi gani kituo hicho ni muhimu kwa mkakati wa kijeshi wa rais Bashar al-Assad. Kama kambi hiyo itaangukia mikononi mwa waasi ambao tayari wanadhibiti mpaka wa kaskazini kuelekea Uturuki, Assad atakuwa anategemea njia moja tu --- kutoka bandari ya Latakia katika bahari ya Mediterranean kwa ajili ya kusafirisha mahitaji muhimu kwa vikosi vinavyopambana kuurudisha mji muhimu wa Aleppo, ambao ndiyo mkubwa zaidi nchini Syria.

Raia wa Syria wakitafuta miili ya watu katika vifusi vya jengo lililoharibiwa katika mashambulizi ya ndege za jeshi la Syria.

Raia wa Syria wakitafuta miili ya watu katika vifusi vya jengo lililoharibiwa katika mashambulizi ya ndege za jeshi la Syria.

Afisa wa zamani wa jeshi la Syria aliyejiunga na waasi, Luteni Kanali Khaled Hamood alisema mapambano ya sasa yalianza siku 11 zilizopita ambapo walienda kama kundi dogo kuikomboa kambi hiyo lakini walishangazwa na upinzani ulioonyeshwa na vikosi vya serikali. Aliongeza kuwa jeshi linapigana kufa na kupona na hawajali kama wanapoteza maelfu ya wanajeshi ili kuendeleza udhibiti wa kituo hicho. Mji wa Maaret al-Numan tayari umeshatekwa na wapinzani hao wa rais Assad, na hivyo kukata njia kuu ya Aleppo. Lakini bila udhibiti wa kituo hicho cha karibu cha kijeshi, udhibiti wao wa barabara hiyo hautakuwa na maana.

Hamood alisema anaamini kundi la wanajeshi wapatao 500 wanailinda kambi ya Wadi al-Daif iliyoko karibu mita 500 kutoka barabara kuu ya kutoka Damascus kwenda Aleppo, wakisaidiwa na mashambulizi ya angani ambayo Assad anayatumia dhidi ya waasi na wakaazi wa Maarat al-Numan. Kambi hiyo pia inaweza kuwa kituo muhimu cha ugavi wa mafuta ikiaminika kuwa na lita milioni 5 za mafuta ya taa katika maghala matano chini ya ardhi. Wanaharakati wanaompinga rais Bashar al-Assad wamesema raia 40 waliuawa katika mashambulizi ya angani Alhamis iliyopita, katika moja ya makabiliano makali zaidi ya mgogoro huo.

Wanajeshi wa Jeshi Huru la Syria, FSA wakiwa katika wilaya ya Salaheddin mjini Aleppo.

Wanajeshi wa Jeshi Huru la Syria, FSA wakiwa katika wilaya ya Salaheddin mjini Aleppo.

Baada ya kuzidiwa katika nchi kavu, jeshi la Syria sasa linawapatia mahitaji wanajeshi waliyoko katika kambi ya Wadi al-Deif kutokea angani likiangusha mikate na vyakula vingine kutoka katika helikopta. Lakini jitihada zake za kuwaongezea vifaa vya kijeshi zimekumbana na upinzani mkali kutoka kwa waasi waliyoizingira kambi hiyo.

Juhudi za mwisho siku ya Jumapili ziliishia kwa vifaru vinne kuharibiwa na kuwalaazimu wanajeshi waliobakia kurudi nyuma. Hamood alisema kama watafanikiwa kuichukua kambi hiyo, watazidisha juhudi za kuzuia njia ya kutoka Latakia kwenda Aleppo, ambayo ni njia kuu ya pili ya ugavi kwa vikosi vya Assad kwenda kaskazini kupitia mji wa Jisr al-Shughour. Wanasema hii itasaidia kuukomboa kabisaa upande wa kaskazini na kuelekeza nguvu upande wa kusini mwa Syria.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre
Mhariri: Saum Yusuf Ramadhan

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com