Sudan yaapa kuikomboa Heglig | Matukio ya Afrika | DW | 14.04.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Sudan yaapa kuikomboa Heglig

Jeshi la Sudan limesema linasonga mbele kuelekea mji wa Heglig kuviondoa vikosi vya Sudan ya Kusini kwenye eneo hilo lenye utajiri wa mafuta, linaloshikiliwa na majeshi ya Sudan ya Kusini kwa siku ya tatu sasa.

Rais wa Sudan, Omar Hassan al Bashir.

Rais wa Sudan, Omar Hassan al Bashir.

Mapigano kati ya Sudan hizo mbili wiki hii yamesababisha mataifa hayo kuwa karibu na vita kamili, ikiwa ni miezi tisa tu baada ya Sudan ya Kusini kujitenga kupitia makubaliano ya amani yaliyomaliza miongo kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Sudan ya Kusini ilichukuwa udhibiti wa eneo la mpakani la Heglig hapo Jumanne (10.04.2012), jambo lililosababisha lawama kali kutoka jumuiya ya kimataifa. Umoja wa Afrika uliuita ukaliaji huo wa kijeshi kuwa ni haramu na kuzitaka pande mbili hizo kujiepusha na vita vinavyoweza kuleta maafa makubwa.

Eneo hilo, ambalo upande wa kusini unasema ni lake, ni muhimu sana kwa uchumi wa Sudan kwani linatoa karibu ya nusu ya mafuta ya nchi hiyo. Maafisa wa serikali ya Sudan wanasema mapigano yamezuia kabisa uzalishaji wa mafuta ghafi katika eneo hilo.

Sudan yaapa kuitwaa tena Heglig

Wapiganaji wa Jeshi la Ukombozi la Sudan.

Wapiganaji wa Jeshi la Ukombozi la Sudan.

Jeshi la Sudan, ambalo limeapa kurudisha mashambulizi ikiwa jeshi la kusini(SPLA) halitajiondoa, limesema kwamba kwa sasa liko kwenye viunga vya Heglig na kwamba linasonga mbele. Msemaji wa jehsi hilo, Al-Sawami Khalid Saad, aliwaambia waandishi wa habari mjini Khartoum kwamba "hali katika eneo la Heglig itatatuliwa hivi punde."

Hata hivyo, msemaji wa jeshi la Sudan ya Kusini, Philip Aguer, alisema hajapokea taarifa zozote za mapigano hadi Ijumaa (13.04.2012) lakini hali ingelifahamika zaidi Jumamosi.

"Ikiwa wanajeshi wa Sudan wanasonga mbele, jeshi la SPLA liko tayari kulipa mipaka yake. Walipoondolewa kwenye eneo hilo ni kwa sababu walikuwa wanalikalia kwa nguvu. Hivyo kama wanataka kurudi kwa nguvu, waache wajaribu." Aguer aliliambia Shirika la Habari la Reuters kwa njia ya simu.

Sudan ya Kusini kujiondoa Umoja wa Mataifa ukiingilia kati

Wapiganaji wa Jeshi la Ukombozi la Sudan.

Wapiganaji wa Jeshi la Ukombozi la Sudan.

Akizungumza na waandhishi wa habari akiwa jijini Nairobi, kiongozi wa Sudan ya Kusini katika mazungumzo ya kumaliza mzozo wa Sudan, Pagan Amum, alisema nchi yake iko tayari kujiondoa kwenye eneo hilo chini ya mpango utakaosimamiwa na Umoja wa Mataifa.

"Tuko tayari kujiondoa Heglig kama eneo hili linalogombaniwa, ikiwa tu Umoja wa Mataifa utapeleka wanajeshi wake katika maeneo haya yanayogombaniwa na pia kuweka utaratibu wa kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano baina ya pande zinazohasimiana."

Amum alisema kuna maeneo saba yanayogombaniwa na akataka kuwepo na upatanishi wa kimataifa kumaliza mzozo juu ya maeneo hayo.

Kuharibiwa kwa mitambo ya mafuta katika eneo la Heglig ni pigo kubwa jengine kubwa kwa Sudan, ambayo tayari inakabiliwa na kupanda kwa bei ya mafuta na kupoteza thamani kwa sarafu yake. Amum alikiri kwamba mitambo hiyo ya mafuta imeathiriwa vibaya, ingawa hakueleza ni kwa kiasi gani.

"Uzalishaji wa mafuta katika eneo hilo utaanza tena pale tu Umoja wa Mataifa utakapopeleka vikosi vyake kati ya nchi mbili na katika maeneo yanayogombaniwa na baada ya mataifa hayo mawili kufikia makubaliano ya kurudisha uzalishaji wa mafuta," alisema Amum.

Sudan ya Kusini yenyewe, ambayo haina mpaka wa bahari, ilizuia uzalishaji wa mapipa 350,000 kwa siku hapo Januari katika mzozo wa kiwango ambacho ilipaswa kulipia kwa kuyasafirisha mafuta ghafi kupitia mabomba na mitambo ya mafuta iliyo chini ya udhibiti wa Sudan. Mafuta yanatoa kiasi ya asilimia 98 ya mapato ya taifa hilo jipya na maafisa wa serikali wamekuwa wakitafuta njia za kufidia pengo hilo.

Mjini Juba, kiasi cha watu 200 waliandamana katika maandamano yaliyoandaliwa na serikali dhidi ya Sudan na kuunga mkono ukaliaji wa Heglig, wakiwa na mabango yaliyosomeka: "Watu wanataka jeshi liwepo Heglig" na "Wanawapiga mabomu watoto na wanawake."

Jumuiya ya Kimataifa yailaani Sudan ya Kusini

Wapiganaji wa makabila kusini mwa Sudan.

Wapiganaji wa makabila kusini mwa Sudan.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo Alhamis (12.04.2012) lilizitaka Sudan na Sudan ya Kusini kuacha mapigano. Balozi wa Sudan katika Umoja huo alisema kwamba Sudan ya Kusini inapaswa kufuata wito huo au vyenginevyo serikali ya Sudan "itaingia ndani kabisa ya kusini."

Umoja wa Afrika, ambao ulikuwa ukisaidia kufanyika kwa mazungumzo ya upatanishi kati ya nchi hizo mbili juu ya malipo ya mafuta na masuala mengine ya yanayobishaniwa kabla ya serikali ya Sudan kujitoa Jumatano iliyopita, pia imeulaani uvamizi na ukaliaji wa kijeshi wa Sudan ya Kusini kwenye eneo la Heglig.

Kamishna wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja huo, Ramtane Lamamra, amesema kwamba baraza lake limechukizwa na kitendo hicho "haramu na kisichokubalika cha majeshi ya Sudan ya Kusini jimboni Heglig, ambalo liko upande wa kaskazini wa mpaka uliokubaliwa tarehe 1 Januari 1956."

Kusini ilijitenga na Sudan mwaka jana, lakini pande hizo mbili hadi sasa hazijakubaliana katika masuala kadhaa likiwemo la mipaka, mgawanyo wa deni la taifa na hadhi ya wananchi wa kila nchi kwa nchi nyengine.

Kiasi cha watu milioni mbili walikufa kwa sababu ya miongo kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, vilivyopiganwa na pande hizo mbili juu ya dini, itikadi, ukabila na mafuta.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters
Mhariri: Stumai George

DW inapendekeza