Vita vyanukia Sudan | Matukio ya Afrika | DW | 12.04.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Vita vyanukia Sudan

Wasiwasi wa kutokea vita kati ya Sudan na Sudan Kusini umetanda baada ya mapigano makali kutokea siku ya jumanne.

Mapigano Sudan

Mapigano Sudan

Hii ni baada ya majeshi ya Sudan Kusini kuliteka eneo la Heglig lenye utajiri mkubwa wa mafuta mpakani mwa nchi hizo mbili na kuwafurumusha wanajeshi wa Sudan kutoka eneo hili linalotambulika kimataifa kama sehemu ya Sudan Kaskazini.

Hatua hii ya Sudan Kusini ililaaniwa na Marekani na Uingereza ambazo kwa pamoja, na Umoja wa Mataifa waliitaka kuondoa majeshi yake katika mji huo lakini pia walilaani kitendo cha Sudan kuishambulia Sudan Kusini kwa kutumia ndege.

Sudan yaonya mashambulizi makubwa zaidi
Balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa, Daffa-Alla Elhag Ali Osman alisema aliwasilisha malalamiko kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulaani uvamizi huu wa Sudan Kusini na kulitaka Baraza hilo liliamrishe nchi hiyo kuondoa majeshi yake.

Osmani aliwaambia waandishi wa habari kuwa kama Baraza la Usalama halitachukua hatua, Sudan itakuwa tayari kujibu mapigo.

Athari za mapigano

Athari za mapigano

"Tunasubiri majibu kutoka Baraza la Usalama. Kama halitachukua hatua kuhusu hali hii, napenda kurudia kwamba sisi tutakuwa tayari kujibu mapigo na tutajibu kwa kishindo kilekile kama wanavyofanya wao," alisema Osma.

Aliongeza kuwa wao kama Sudan wanafahamu kuwa Sudan Kusini ni nchi changa na ina matatizo makubwa na kwa hivyo hawangependa kuzidisha matatizo ya nchi hiyo kwa vile kufanya hivyo hakutakuwa na mafunaa kwa nchi yeyote.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon alisema amestushwa na kuzidi kwa mapigano baina ya nchi hizo mbili na kuzitaka kila mmoja iondoe majeshi yake katika eneo la mwenzie.

Marekani warudi kwenye meza ya mazungumzo
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Victoria Nuland alisema Marekani imesikitishwa sana na hatua ya nchi hizo kupigana lakini akailaumu Sudan ya Kusini kwa kupeleka vikosi vyake katika jimbo la Sudan la Kordofan na kuteka eneo hilo lenye utajiri wa mafuta.

Nuland alisema uvamizi wa Sudan Kusini ulienda mbali zaidi ya haja ya kujilinda na kuzitaka nchi zote zisitishe mapigano mara moja bila ya masharti yoyote, na pia ziache kuunga mkono makundi yenye silaha yanayopambana na serikali upande mwingine..

Wanajeshi wakiwa katika jimbo la Abyei

Wanajeshi wakiwa katika jimbo la Abyei

Aliwaomba marais wa nchi hizo mbili wakubali kukutana kama ilivokuwa imepangwa hapo awali, ili kujadili na kufikia mwafaka juu ya masuala yanayozuia kuwepo kwa amani ya kweli baina ya nchi hizo mbili.

Chini ya mkataba wa amani wa mwaka 2005, nchi hizo zinatakiwa zimalize tofauti zilizobakia juu ya mgawanyo wa mapato yatokanayo na mafuta na pia kuainisha vizuri mipaka baina yake

Umoja wa Afrika wanena
Umoja wa Afrika ulisema ulistushwa na kuongeza kwa vurugu baina ya nchi hizi mbili lakini jitahada zake za kusuluhisha zilipata pigo baada ya Sudan kukasirika na kujiondoa katika mazungumzo ya amani.

Sudan inasema hatua ya Kusini kuteka eneo lake ndiyo ukiukwaji mkubwa wa uhuru wa mipaka yake.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\APE\AFPE
Mhariri: Saum Yusuf