1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan Kusini yaadhimisha miaka 3 ya kujitenga

8 Julai 2014

Sudan Kusini inaadhimisha miaka mitatu tangu ijipatie uhuru wake kutoka Sudan katika wakati ambapo nchi hiyo ndogo iko kwenye hali ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyojengeka kwa misingi ya kikabila

https://p.dw.com/p/1CYIx
Picha: dapd

Sudan Kusini inashuhudia mauaji pamoja na kitisho cha kutumbukia katika janga la ukame.Licha ya utajiri mkubwa wa mafuta pamoja na msaada wa mabilioni kutoka kwa wafadhili wakigeni bado Sudan Kusini inaorodheshwa miongoni mwa nchi zilizoshindwa kabisa.

Utafiti wa hivi karibuni kabisa uliochapishwa na shirika la linalofuatilia masuala ya amani la Fund for Peace umeiweka nchi hiyo ndogo ya Sudan Kusini katika nafasi ya juu kwenye orodha ya nchi zinazokabiliwa na hali tete ikizitangulia Somalia,Afghanistan na Iraq.Katika mji mkuu Juba barabarani unachokumbana nacho ni mabango yenye ujumbe unaodai kwamba wasudan Kusini ni kitu kimoja na taifa moja, lakini vita vinavyoendelea kushuhudiwa kote kwenye taifa hilo na kiasi ya robo yano ya idadi jumla ya watu wa taifa hilo wakiwa wamelazimika kuishi kama wakimbizi,suala la kufanyika mazungumzo yoyote ya kuleta umoja wa Kitaifa likionekana kama limeshindikana ni wazi kwamba ni machache yatakayowafanya watu wa nchi hiyo washerehekee kumbukumbu hiyo.

Sudan Kusini ilipotangaza uhuru wake kamili mwaka 2011
Sudan Kusini ilipotangaza uhuru wake kamili 2011Picha: picture-alliance/dpa

Mji mkuu Juba umegawika tangu mwezi wa Desemba wakati walinzi wa rais wanaomuunga mkono rais Salva Kiir walipoingia kwenye mapambano na vikosi vinavyomuunga mkono makamu wa rais wa zamani Riek Machar kitendo kilizusha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ambayo sasa yamefikia miezi saba.Mapigano ya mwanzo yalisababisha mamia ya watu kutoka kabila la Nuer ambalo anatokea bwana Machar kuuwawa kinyama na wanajeshi pamoja na watu kutoka kabila la Dinka,kabila ambalo ni kubwa nchini humo na analotokea rais Salva Kiir.

Maelfu ya wengine walilazimika kuyatoroka makaazi yao na kukimbilia Juba kwenye kambi ya Umoja wa Mataifa ambako hadi sasa wanaishi katika msongamano huku kambi hiyo ikiwa imewekwa uzio na kulindwa na wanajeshi wa kuweka amani wa Umoja wa Mataifa.Katika miji mingine maelfu ya watu wa kabila la Dinka wameachwa bila makaazi kutokana na hatua za kulipiza kisasi zinazochukuliwa na wapiganaji wanuer ikiwa ni pamoja na mauaji,ubakaji,uporaji na kuharibu mali za wadinka.

Gatmai Nhial Riek mwanafunzi mwenye umri wa miaka 26 kutoka kabila la Nuer anayeishi kwenye kambi ya Umoja wa Mataifa mjini Juba tangu miazei sita iliyopita anawalaumu watu wa kabila la Dinka akisema kuishi kwao kambini kumesababishwa na mauaji yanayofanywa na Dinka dhidi yao.Wengi kwahivyo wanaogopa kusafiri kwenye vijijini mwao ambako wanakutikana watu wa makabila yao kutokana na khofu ya kuvamiwa.

Lakini kwa baadhi walioko kwenye mji mkuu wa nchi jirani ya Sudan,Khartoum maisha ni ya kuvutia kiasi.Kijana Abrahama Tut Mayak Kai mwenye umri wa miaka 27 anasema ni bora kuishi mjini Khartoum kuliko Sudan Kusini.Anasema hali ya usalama inatisha hasa kwa wanuer katika Sudan Kusini ingawa pia anakiri mjini Khartoum wanaangaliwa kama wageni na sio raia kwakuwa nchi hizo mbili zimetengana.

Sudan Kusini iliundwa baada ya muda mrefu wa vita na mapambano ya kudai uhuru kutoka Khartoum na hatimae ilifanikiwa kupepeprusha kwa mara ya kwanza bendera yake ya uhuru mwaka 2011 katika sherehe za kutambulika kimataifa huku kukiweko matumaini makubwa hasa kutokana na kwamba sehemu kubwa ya utajiri wa Mafuta uliiangukia nchi hiyo sambamba na misaada mikubwa ya jumuiya ya Kimataifa.

Riek Machar na Salva Kiir 09.07.2013
Picha: Reuters

Lakini kwa watafiti na wachambuzi kama Zacharia Diing Akol kutoka taasisi huru ya utafiti ya Sudan Kusini SUDD,hali halisi inayoshuhudiwa sasa katika taifa hilo haina tofauti kubwa na hali iliyokuweko miaka mitatu iliyopita.Mtafiti huyo akikumbuka mafanikio ya harakati za kudai uhuru anasema mwaka 2011 ulikuwa mwaka wa furaha na matumaini kwa kila raia wa Sudan Kusini huku kila mmoja akijihisi kupata hadhi kama raia wa taifa hilo na kuwa na imani kwamba ataishi bila ya khofu katika taifa lake lakini mambo yamebadilika ghafla na wengi kupoteza maisha yao.Si hayo tu lakini pia tayari mashirika ya miaada yanasema ukame unainyemelea nchi hiyo kwa karibu sana na maisha ya kiasi watu milioni 4 yatakuwa hatarini ikiwa fedha za msaada wa chakula hazitotolewa.

Mwandishi Yusuf Saumu

Mhariri:Mohammed AbdulRahman.