Sudan: Al-Bashir huenda amejiuzulu, jeshi kutoa taarifa
11 Aprili 2019Maelfu ya wakaazi wa mjini Khartoum waliimba, "utawala umeanguka" wakati wakimiminika katika eneo kuzunguka makao makuu ya jeshi ambako waandamanaji wamekuwa wakikaa hapo kwa muda wa siku sita sasa.
"Jeshi la Sudan litatoa taarifa muhimu hivi karibuni. Subirini, mtangazaji wa televisheni ya taifa alisema, bila ya kutoa maelezo zaidi. Mtu ambaye haikuelezwa ni nani alisema.
"Watazamaji wa televisheni ya Sudan , katika muda mfupi ujao jeshi litatoa taarifa muhimu"
Muziki wa kijeshi umechukua nafasi ya matangazo ya kawaida katika televisheni. 'Hatutaondoka hapa hadi tutakapofahamu ni kitu gani jeshi litatuambia. Lakini tunafahamu kwamba Bashir lazima aondoke. Tunasubiri taarifa muhimu,' mmoja kati ya waandamanaji aliliambia shirika la habari la AFP kutoka katika eneo ambalo waandamanaji wamekita kambi. Tumechoshwa na utawala huu , miaka 30 ya ukandamizaji, rushwa , ukiukaji wa haki za binadamu, imetosha, amengeza mtu huo.
Maandamano, ambayo yalizuka Desemba, yamekuwa changamoto kubwa hadi hivi sasa katika utawala wa miongo mitatu wa Bashir wa mkono wa chuma.
Kundi la wandamanaji limekuwa likiishi kwa siku tano nje ya makao makuu ya jeshi, eneo ambalo pia ni makao rasmi ya rais Bashir na wizara ya ulinzi.
Kumekuwa na hali ya sherehe katika eneo hilo, ambalo waandamanaji wanaimba na kucheza nyimbo za kimapinduzi.
Magari kadhaa ya kijeshi yakiwa na wanajeshi yaliingia katika eneo hilo la jeshi mapema leo , kwa mujibu wa watu walioshuhudia.
Wamesema magari mengi ya jeshi yakiwa na wanajeshi yamewekwa katikati ya Khartoum mapema leo.
kundi linaloongoza maandamano ya nchi nzima limewataka wakaazi wa mji mkuu Khartoum na kwingineko kujazana nje ya makao makuu ya jeshi. Mtandao wa televisheni za mataifa ya Kiarabu ulitangaza ripoti ambazo hazijathibitishwa kwamba Omar al-Bashir amejiuzulu na kwamba maafisa wa ngazi ya juu wa chama tawala pia wanakamatwa.
Mahali alipo kiongozi huyo dikteta , ambaye ametengwa na mataifa mengi na pia anatakiwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu kwa mauaji katika jimbo la Darfur, bado hakujulikani.