Somaliland yafanya uchaguzi wa kwanza tangu 2005 | Matukio ya Afrika | DW | 31.05.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Somaliland yafanya uchaguzi wa kwanza tangu 2005

Watu wa Somaliland wanapiga kura katika uchaguzi wa bunge na serikali za mitaa, unaoashiria kupigwa hatua katika mkoa huo wa Somalia wenye utawala wa ndani ambao kwa miaka mingi umeepuka machafuko mabaya ya nchi hiyo

Zaidi ya watu milioni moja kati ya milioni nne wanaoishi Somaliland wamesajiliwa kupiga kura. Jimbo hilo limewaalika waangalizi kufuatilia uchaguzi huo, wakiwemo viongozi wa kisiasa kutoka maeneo mengine ya Afrika.

Mwanaharakati wa kupambana na rushwa kutoka Kenya John Githongo ambaye yuko katika mji mkuu wa Somaliland Hargeisa, kama mwangalizi, ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa mkoa huo ni moja ya maneneo ya Somalia ambalo demokrasia inayoanzia chini kwa wananchi wa kawaida kwenda juu kwa viongozi inaonekana kufanya kazi.

Somaliland Reportage Verkehr in Hargeisa

Mji Mkuu wa Somaliland Hargeisa una utulivu

Greg Mills, mkurugenzi wa shirika moja la Afrika Kusini linalouangalia uchaguzi huo, amesema katika taarifa kuwa Eneo hilo lenye utawala wa ndani ni mfano wa nchi ya Afrika inayoheshimu demokrasia na maendeleo na linahitaji uungwaji mkono wa kila Muafrika anayetaka kuona maendeleo ya bara la Afrika.

Somaliland ilijitenga na Somalia mwaka wa 1991 wakati nchi hiyo ilitumbukia katika mgogoro ulioongozwa na wababe wa kivita. Licha ya kukosa kutambuliwa kimataifa, Somaliland inajiendesha kwa serikali yake yenyewe, sarafu na mfumo wa usalama.

Somalia inaizingatia Somaliland kuwa sehemu ya himaya yake. Duru kadhaa za mazungumzo kuhusu uwezekano wa kuungana zimeshindwa kufikia makubaliano na jimbo hilo linaendelea kudai haki yake ya uhuru.

Ni mara ya kwanza kwa uchaguzi wa kitaifa na wa serikali za mitaa kufanywa kwa pamoja, huku mistari mirefu ikiripotiwa katika baadhi ya vituo vya kupiga kura.

Somalia Präsident Mohamed Abdullahi Mohamed | Farmajo

Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed Farmajo

Rais Muse Bihi Abdi na viongozi wa vyama viwili vya upinzani vya Somaliland wamehimiza uchaguzi wa amani baada ya kupiga kura zao katika mji mkuu Hargeisa.

Uchaguzi wa rais unaandaliwa tofauti na utafanyika baada ya muhula wa miaka mitano wa Rais Muse utakamilika mwishoni mwa 2022.

Wapiga kura wa kuanzia umri wa miaka 15, wamepewa jukumu la kuwachagua viongozi wao kutoka kwa orodha ya watu 250 wanaogombea viti 82 vya bunge na karibu 1,000 wanaotafuta nyadhifa 249 za udiwani.

Mogadishu na viongozi wa mikoa mitano ya Somalia yenye utawala wa ndani mwezi huu walikubaliana kuandaa uchaguzi uliocheleweshwa kwa muda mrefu katika siku 60, baada ya ratiba ya awali kuvunjika kwa sababu ya machafuko. Uchaguzi huo sio wa moja kwa moja, kama tu ilivyokuwa katika uchaguzi wa awali, ambapo wajumbe maalum huteuliwa na viongozi wa koo ili kuwachagua wabunge, ambao nao watamchagua rais.

AFP, AFPE, Reuters