Silvio Berlusconi ahukumiwa miaka saba gerezani | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.06.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Silvio Berlusconi ahukumiwa miaka saba gerezani

Waziri mkuu wa zamani wa Italia, Silvio Berlusconi, jana Jumatatu alihukumiwa kifungo cha miaka saba gerezani na kupigwa marufuku kushiriki katika siasa maishani kwa mashitaka ya kuwalipa makahaba wa umri mdogo

Hukumu hiyo ni pigo kubwa kwa Berlusconi mwenye umri wa miaka 76 ambaye ameshitakiwa mara chungu nzima kuhusiana na shughuli zake za kibiashara lakini hakuwahi kushitakiwa kutokana na mienendo ya kuhusu maisha yake ya kibinafsi.

Licha ya hayo, mwanasiasa huyo ameapa kuwa siku zake kisiasa hazijafikia ukingoni. Ana fursa ya kukata rufaa na punde baada ya hukumu hiyo kutolewa wafuasi wake walimzingira ili kumuunga mkono.

Mashitaka hayo yanatokana na sherehe alizokuwa akizifanya alipokuwa waziri mkuu wa Italia katika jumba lake la kifahari mjini Manilla mwaka 2010 ambako wasichana warembo walialikwa kunywa na kustarehe naye na zilijipatia jina maarufu la 'bunga bunga.'

Karima El Mahrough anayehusishwa na kesi ya ngono inayomkabili Berlusconi

Karima El Mahrough anayehusishwa na kesi ya ngono inayomkabili Berlusconi

Upande wa utetezi ulisema sherehe hizo zilikuwa za kifahari lakini za heshima ilhali upande wa mashitaka ulisema ziliandaliwa kwa lengo la kukidhia ngono na wasichana walilipwa hela kuzihudhuria.

Sakata ya ngono yamtia matatani

Mwanamke anayejikuta katikati mwa kashfa hii, Karima el Mahroug kwa jina jingine Ruby, amesema wasichana walioalikwa walikuwa wanamvulia nguo Berlusconi kwa njia ya kumvutia. Berlusconi na el Mahroug wote wamekanusha madai kuwa walishiriki ngono na msichana huyo amekanusha kuwa aliwahi kufanya kazi kama kahaba.

Baada ya hukumu hiyo, Berlusconi aliandika katika ukurusa wake wa facebook kuwa anaamini ataondolewa mashitaka kwa sababu kutokana na hali ilivyo, hakuna uwezekano wa kumfunga na kuongeza kuwa ni njama ya kumbandua kutoka ulingo wa siasa za Italia.

Hukumu hiyo haikutarajiwa na kujumuisha masuala ambayo hayakuwa katika mashitaka ya mwanzo na kuhoji wazi iwapo wengi wa wasichana waliotoa ushahidi waliidanganya mahakama ili kumlinda Berlusconi.

Jopo la majaji Italia waliomhukumu Berlusconi

Jopo la majaji Italia waliomhukumu Berlusconi

Uchunguzi zaidi kufanywa

Jopo la majaji watatu wote wa kike lilisema waziri mkuu huyo wa zamani alivuka mipaka ya ushawishi wake ili kuficha uhusiano na msichana mwenye asili ya Morroco wa umri wa miaka 17 na kwamba aliingilia kati ili aachiliwe kutoka rumande ya polisi aliposhitakiwa kwa wizi na kutokana na hilo, walimuongezea mwaka mwingine mmoja zaidi iliyokuwa imetakiwa na upande wa mashitaka.

Mahakama pia imesema itaangalia faili za waendesha mashitaka zilizo na ushahidi wa zaidi ya wasichana 30 waliohudhuria sherehe hizo za bunga bunga kuchunguza iwapo walidanganya licha ya kula kiapo walipokanusha kuwa lengo la sherehe hizo lilikuwa ni ngono.

Masaibu ya Berlusconi bado hayajaishia hapo kwani anakabiliwa na rufaa ya mwisho kwa kushitakiwa kwa udanganyifu wa kodi ambapo alihukumiwa miaka minne gerezani na marufuku ya miaka mitano ya kushikilia wadhifa wa uongozi.

Mwandishi:Caro Robi/ap/afp

Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com