Silaha ndogo ndogo zasababisha madhara makubwa kijamii | NRS-Import | DW | 15.07.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

NRS-Import

Silaha ndogo ndogo zasababisha madhara makubwa kijamii

Ma mia ya maelfu ya silaha ndogo ndogo hupotea na mara nyingi huishia mikononi mwa makundi ya waasi katika nchi kama Irak, Afghanistan na Colombia. Juhudi za kuondoa sihala mikononi mwa raia zinakabiliwa na vizingiti.

default

Shehena ya silaha zilizokamatwa Somalia kutoka kwa raia

Kulingana na ripoti ya mwaka huu ya Shirika la uchunguzi wa silaha ndogo ndogo la Small Arms Survey lenye makao yake mjini Geneva Usuisi, kiasi ya silaha ndogo ndogo laki 6,5 zinazomilikiwa na raia hukosekana kila mwaka.

Takwim hizo hazijazingatia idadi kubwa ya silaha zinazopotoshwa kutoka ghala za serikali na jeshi na kutajwa kwamba ziliibiwa na kupatikana kwenye soko haramu.

Kupotoshwa silaha hizo ni hatari kwa sababu kunaweza kukapelekea silaha kuzagaa miongoni mwa raia na makundi ambayo yanaweza kudhuru maisha ya raia wengine, amesema Keith Krause, mkuu wa Shirika hilo la uchunguzi juu ya silaha ndogo ndogo wakati akitoa ripoti yake ya mwaka huu mjini New York Marekani.


Krause amezitolea mwito serikali na jeshi katika nchi kuwa waangalifu sana ili kuhakikisha kwamba silaha zao ndogo ndogo hazikabidhiwi waasi au makundi yasiokuwa ya kiserikali kinyume cha sheria.

Hata hivyo, Shirika hilo halikutoa makisio ya silaha na zana za kijeshi zinazotoweka kutoka ghala za serikali na jeshi. Lakini kuhusu Kenya, ripoti hiyo inasema kati ya asili mia 40 na 50 ya silaha na zana za kijeshi zinazopatikana kwenye soko la magendo, zilitoka katika ghala za jeshi na polisi. Kumekuwa na juhudi za kuondoa silaha zinazomilikiwa na raia kinyume cha sheria katika nchi karibu zote, ila tatizo ni kwamba hakuna ushirikiano kati ya nchi kulisuluhisha swala hilo.


Mbali na ukosefu wa ushirikiano kati ya nchi, kikwazo kingine ni kuendelea kwa vita katika nchi mbali mbali kama vile Irak na Afghanistan na nchi ambazo zinazo silaha za ziada ambazo hazihitajiki, huziuza badala ya kuziteketeza, limesema Shirika hilo la uchunguzi juu ya silaha ndogo ndogo. Shirika hilo linatoa mfano kwamba juu ya silaha laki 7,5 zilizouziwa idara za usalama nchini Irak na Afghanistan tangu vita vianze katika nchi hizo miaka ya 2003 nchini Irak na 2001 nchini Afghanistan, ang'alau nusu milioni zilikuwa zimeshatumiwa na zingestahili kuteketezwa badala ya kuuzwa.

Silaha ndogo ndogo kiasi ya laki 4,3 kutoka mikononi mwa raia huteketezwa kila mwaka duniani kulingana na ripoti hiyo ambayo inaongeza kusema kuwa juu ya silaha ndogo ndogo kiasi ya milioni 200 duniani, milioni 76 ni za ziada lakini hazijateketezwa. Inaelekea agizo la kuharibu silaha za ziada lililotolewa mara tu baada ya kumalizika vita vikuu vya pili vya dunia halifuatwi.

Kulingana na Aorn Karp, mtaalamu katika Shirika hilo la uchunguzi juu ya silaha ndogo ndogo, Marekani inahimiza nchi kuteketeza silaha zao za ziada lakini wakati huo huo, huzishawishi kuuza silaha zao katika nchi zinazokabiliwa na vita kama Irak au Afghanistan na kudumisha tatizo hilo la udhibiti wa silaha ndogo ndogo.


 • Tarehe 15.07.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Eco5
 • Tarehe 15.07.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Eco5
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com