Siku ya kupambana na Ukimwi-Vijana ndio wanaotishiwa zaidi | Afya na masuala ya kijamii | DW | 01.12.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Afya na masuala ya kijamii

Siku ya kupambana na Ukimwi-Vijana ndio wanaotishiwa zaidi

Leo ni siku ya kimataifa ya kupambana na UKIMWI. Kenya inafanya juhudi mpya baada ya takwimu rasmi kuonyesha kuwa 51% ya maambukizi mapya yanatokea miongoni mwa vijana walio na umri wa miaka ya 15-24

Ripoti ya Baraza la kitaifa la kupambana na Ukimwi nchini Kenya, NACC inatahadharisha kuwa maambukizi ya makundi mengine ya jamii mbali na vijana, hayajaongezeka wala kupungua. Inasadikika kuwa hofu ya kupimwa na tabia za kufanya mapenzi kiholela ni baadhi ya vyanzo vya maambukizi mapya katika vijana. 

Kulingana na ripoti ya baraza la kitaifa la kupambana na ukimwi maambukizi mapya kati ya vijana yameongezeka tangu mwaka uliopita.Kwa kila watu 5 wanaoambukizwa wawili ni vijana walio na umri wa kati ya miaka 15-24. Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya watu alfu 26 walioripotiwa kuambukizwa virusi vya HIV mwaka uliopita,alfu tatu kati yao walifariki dunia kwa sababu ya matatizo yanayotokana na ugonjwa wa Ukimwi.

Kulingana na mkuu wa mpango wa kitaifa wa kupambana na Ukimwi na magonjwa ya zinaa,NASCOP, Kigen Barmasai, takwimu hizo zinatia hofu.Inasadikika kuwa vijana wengi wanafanya mapenzi kiholela kwa sababu ya ulevi na uraibu wa mihadarati au pia kushindwa kukataa kwa sababu moja au nyengine.

Kukosekana kwa elimu ya afya ya uzazi ni tatizo

 HIV / AIDS-Test in Gaza (06.01.2017) (Provinz -sud Mosambik)
(DW/C. Matsinhe)

Bado vijana wengi wanaogopa kwenda kuchukua vipimo vya HIV

Changamoto kubwa ni ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi na haki zinazoambatana na mazingira hayo.Vijana wanaaminika kuchelea kupimwa kujua iwapo wameambukizwa virusi vya HIV ambayo ndiyo hatua ya kwanza ya kupambana na maambukizi.Takwimu zinaashiria kuwa vijana huanza kufanya mapenzi kwa mara ya kwanza kabla ya kutimiza umri wa miaka 15.Kadhalika 67% ya wasichana ndio hutumia mipira ya kondomu kwa mara ya kwanza wanapojuana kimwili na wavulana.Wavulana ni wachache Zaidi wanaotumia mipira ya kondom kwa mara ya kwanza kwani takwimu zinaonyesha ni 58%.

Jambo jengine la kutia hofu ni kuwa vijana hawa hubadili mienendo na kuacha kutumia mipira ya kondom kadri wanavyoendelea hata wanapofanya mapenzi na watu wasiojuana nao vizuri.Suluhu ni wazazi kuwa chonjo kuwashauri na vijana wenyewe kupata elimu ya kutosha ya afya ya uzazi na haki zao.

Umasikini pia wanyoshewa kidole

Durban AIDS Konferenz Südafrika (Getty Images/R.Jantilal)

UKIMWI ni miongoni mwa magonjwa yanayowauwa watu wengi zaidi barani Afrika

Hali hii inachangia katika mimba za mapema na matatizo ya afya ya uzazi.Mtaala wa kitaifa nao pia unanyoshewa kidole cha lawama kwa kujikita zaidi kwenye masomo yanayotahiniwa pekee na kutelekeza umuhimu wa elimu ya masuala ya jamii hususan afya ya uzazi na uhusiano kati ya wavulana na wasichana. Ukosefu wa uelekezi nao pia unawapotosha vijana vilevile umasikini unawasukuma kwenye ukahaba na tabia zisoridhisha. Hata hivyo teknolojia sasa inamuwezesha aliyeambukizwa virusi vya HIV kwa bahati mbaya kupewa mchanganyiko wa dawa za kuzuwia madhara maarufu Prep.Elimu inahitajika kuepusha matumizi mabaya ya kinga hii.

Kwa sasa shirika la afya uliomwenguni WHO linaiweka idadi ya wanaoishi na virusi vya HIV kuwa milioni 36.7.Kauli mbiu ya mwaka huu ni haki ya afya: na kuwa ni wajibu wa kila mmoja kupambana na Ukimwi.Kutoka Nairobi mimi ni Thelma mwadzaya

Mwandishi: Thelma Mwadzaya

Mhariri: Josephat Charo
 

 

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com