Sigmar Gabriel afanya ziara ya ghafla Somalia | Matukio ya Afrika | DW | 02.05.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Sigmar Gabriel afanya ziara ya ghafla Somalia

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel ameahidi msaada maradufu kwa nchi ya Somalia ambayo imekumbwa na ukame.

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani pia ameonya juu ya janga la kibinaadamu linaloweza kuwakumba raia zaidi ya milioni 6 nchini Somalia ambao wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula. 

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel aliwasili mjini Mogadishu huku kukiwa na ulinzi mkali. Waziri Gabriel ametangaza msaada utakaotolewa na serikali ya Ujerumani kwa Somalia ambao ni Euro milioni 70 sawa na Dola milioni 76 za Kimarekani. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani pia ameitaka jamii ya kimataifa iongeze juhudi za kupambana na njaa ya nchini Somalia. Janga la njaa la mwaka 2011 nchini Somalia lilisababisha vifo vya watu zaidi ya laki mbili na nusu.

Außenminister Gabriel besucht Somalia (picture alliance/dpa/M.Gambarini)

Ni ziara ya kwanza ya waziri wa Ujerumani nchini Somalia

Hata hivyo wakati waziri Gabriel alipokuwa akitangaza msaada wa Ujerumani kwa serikali ya Somalia, aliitaka nchi hiyo ijitahidi kupunguza kutegemea misaada.  Gabriel alisema ni jambo la kutia moyo kuona Somalia sasa ina serikali na rais.  Alisema nchi hiyo ina nafasi nzuri sasa ya kufanya mabadiliko. Waziri mkuu wa Somalia Hassan Ali Khaire amesema nchi yake bado inahitaji misaada na hali hiyo ni ya muda mrefu hadi pale itakapoweza kujisimamia vyema.

Ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani haikutangazwa kutokana na sababu za kiusalama.  Somalia inakabiliwa mara kwa mara na mashambulio kutoka kwa kundi lenye itikadi kali za Kiislamu la Al Shabaab. Mnamo mwaka 1991 aliyekuwa rais wa nchi hiyo Mohamed Siad Barre alipinduliwa na kutokea hapo nchi hiyo imetumbukia kwenye machafuko.  Serikali zilizoundwa kutokea mwaka 2004 zilijaribu kuweka mamlaka yao lakini zilikabiliwa na vitisho vikubwa kutoka kwa kundi la Al Shabaab.

Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Farmajo aliyechukuwa hatamu za uongozi mnamo mwezi Februari ameahidi kuendeleza mapambano dhidi ya kundi hilo la Al Shabaab. Waziri Sigmar Gabriel atakutana na watu waliopoteza makaazi yao na wale waliokuwa zamani wapiganaji wa kundi la Al Shabaab. Ziara ya waziri wa mambo ya nje Sigmar Gabriel nchini Somalia ni ya kwanza katika nchi hiyo ya pembe ya Afrika kuwahi kufanywa na waziri wa Ujerumani.

Mwandishi: Zainab Aziz/DPAE

Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com