1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shughuli za umma na zile za kisiasa zaanza kurejea Kenya

Wakio Mbogho20 Julai 2020

Mikutano ya kisiasa na shughuli zingine za umma nchini Kenya zimerejelea hali ya kawaida licha ya kuwepo kwa masharti ya kudhibiti utangamano unaolenga kuyakabili maambukizi ya virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/3fafW
Alkoholismus in Afrika
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Inganga

Ongezeko la idadi ya maambukizi inaonekana kuilemea wizara ya afya, ambayo kwa siku kadhaa sasa imekuwa ikirekodi zaidi ya maambukizi mia sita kwa siku. 

Eneo la magharibi mwa Kenya, ambalo katika siku za hivi karibuni limekuwa uwanja wa kisiasa kati ya mababe wa upinzani na wandani wa naibu Rais William Ruto limekuwa likishuhudia misururu ya mikutano ya kisiasa licha ya amri ya kutotangamana kwa zaidi ya watu 15. Wanasiasa, magavana na mawaziri ni kati ya viongozi wanaoonekana kutozingatia masharti yaliyowekwa kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa COVID 19. Hata kwenye sehemu za burudani, watu wanaonekana kujivinjari hadi masaa yasiyofaa bila kutatizwa na hatari inayowakodolea macho.

Muda mfupi uliopita Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja amejiwasilisha katika kituo cha polisi cha Kilimani kuandikisha ripoti kuhusiana na tukio la wikendi akituhumiwa kuwa alikiuka masharti kwa kujivinjari kwenye baa kupita muda wa saa tatu usiku uliowekwa. Sakaja ameomba radhi na kutangaza kuwa amejiuzulu kama mwenyekiti wa kamati ya bunge la seneti inayosimamia udhibiti wa ugonjwa wa COVID 19.

Kenia Coronavirus  Uhuru Kenyatta Meeting
Rais Uhuru Kenyatta na baraza la usalama la taifaPicha: PSCU

Juhudi za kukabiliana na ugonjwa huu zinaonekana kuwa kibarua kigumu hasa kwa wizara ya afya. Idadi kubwa ya maambukizi imeshuhudiwa baada ya Rais Uhuru Kenyatta kulegeza baadhi ya masharti na kuruhusu watu kuingia na kutoka katika miji ya Nairobi na Mombasa na hata kufikia zaidi ya watu mia sita kwa siku. Watu wameichukua hii kuwa idhini kwao kulegeza masharti kwenye uchukuzi wa umma na hata kwenye sherehe za kijamii.

Kaunti zote 47 zilitakiwa ziwe na uwezo wa zaidi ya vitanda 300 vya wagonjwa mahututi kwenye hospitali zao. Hii haijawezekana hadi kufikia sasa na licha ya serikali kuahidi kwamba katika muda wa wiki chache ni jambo litakalokuwa limefikiwa bado hali hii imesalia kizungumkuti. Mwenyekiti wa baraza la magavana Wycliffe Oparanya amependekeza kufungwa kwa baadhi ya miji akisema baadhi ya kaunti zinalemewa na ongezeko la maambukizi kwenye kaunti zao.

Wakio Mbogho, DW, Nakuru