Shinikizo lazidi kumuelemea Xabi Alonso
11 Desemba 2025
Alonso amesema anaamini klabu hiyo itarejea kwenye kiwango chake cha kawaida hivi karibuni. Miamba hao wa Uhispania wamepata ushindi katika mechi mbili tu kati ya nane zilizopita katika mashindano yote.
Matokeo hayo yameongeza shinikizo kwa Alonso huku vyombo vya habari nchini humo vikiripoti juu ya kuwepo kwa mvutano kati ya kocha huyo na baadhi ya wachezaji, ingawa baadhi wamejitokeza hadharani na kuonyesha kumuunga mkono.
Mpambano kati ya Madrid na City ndio ulikuwa mkali zaidi wa raundi hiyo katikati ya ripoti kwamba Alonso alikuwa anakabiliwa na kitisho cha kupoteza udhibiti wa wachezaji wake, hali inayoongeza uvumi kuhusiana na kuendelea kusalia kwenye nafasi yake.
Kulishuhudiwa vijembe na kejeli ndani ya Bernabeu baada ya filimbi ya mwisho kulia.
"Tunajua ni wakati mgumu kwetu na kwa kocha," winga wa Madrid Rodrygo alisema. "Mambo hayaendi kama tunavyotaka na nilitaka kuonyesha kwamba tuko nyuma ya kocha wetu. Nilitaka kuonyesha. kwamba tuko pamoja na tunahitaji kuwa na umoja ili kuendelea kusonga mbele na kufikia malengo yetu."
Klabu ya Arsenal inaendelea kushika kasi katika mashindano ya msimu huu hasa baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya Club Brugge, huku bingwa mtetezi Paris Saint-Germain ikimaliza bila ya kufungana na Athletic Bilbao.
Kwingineko, klabu inayoshiriki ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga, Bayer Leverkusen imetoka sare ya 2-2 na Newcastle United katika mchezo wa kusisimua wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Alejandro Grimaldo alifunga bao dakika ya 88 ya mchezo na kuhakikisha wanagawana alama na Newcastle.