1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sheria kuwabana wauaji wa wanaharakati Iraq?

2 Juni 2021

Baada ya kipindi kirefu cha mauaji ya zaidi wapigania demokrasia 30 nchini Iraq, hatimaye mmoja wa washukiwa ametiwa mbaroni. Lakini pamoja na hatua hiyo bado maelfu ya wanaharakati wameendelea kuishi kwa wasiwasi.

https://p.dw.com/p/3uMdT
Irak Bagdad | Demonstration am Tahrir-Platz
Picha: AHMAD AL-RUBAYE/AFP/Getty Images

Kwa miezi kadhaa sasanchini Iraq, wanaharakati, wachambuzi na waandishi wa habari, kwa ujumla yeyote ambae amekuwa akizungumza waziwazi kupigia chapuo mabadiliko ya kisiasa nchini humo anakuwa katika hali ya hatari.

Kwa mujibu wa rekodi za asasi za kupigania haki za binaadamu katika kipindi cha miezi 18 kumekuwepo na vifo vya zaidi ya wanaharakati 35 na majaribio ya mauaji 18. Hayo yametokea tangu kuanza kwa vuguvugu la maandamano maarufu, 2019 ambalo lililazimisha mabadiliko ya kiuongozi.

Serikali ya Iraq imetoa ahadi ya kuvifanyia uchunguzi vitendo vya mauwaji, lakini hadi sasa hakuna chochote kilichofanyika. Miongoni mwa waliokufa wamo wanaharakati maarufu kama Ihab al-Wazni, ambae alikuwa akiratibu maandamano katika mji wa kusini mwa Iraq wa Karbala.

Soma pia: Papa Francis ahimiza jamii za Iraq kuvumiliana

Aliuwawa kwa kupigwa risasi mwanzoni mwa mwezi uliopita. Mwezi Juni mwaka jana aliuwawa mchambizi maarufu wa masuala ya usalama Hisham al-Hashimi, katika tukio ambalo liligonga vichwa vya habari vya ulimwengu.

Irak Protesten nach dem Tod von Ihab al-Wazni
Waandamanaji wakiwa wamebeba jeneza la Ihab al-Wazni wakati wa msiba wake, Mei 9, 2021.Picha: Mohammed Sawaf/AFP

Wanaharakati wengine maarufu, kama Ali Jasb Hattab Aboud, ambae ni mwanasheria mbobezi katika masuala ya haki za binaadamu, ambae alikuwa akitoa usaidizi wa kisheria kwa waandamanaji, ametekwa nyara na hajaweza kuonekana tena hadi leo. Katika jambo linalosikitisha zaidi miongoni mwa waliuwawa yumo baba wa Aboud, ambae alikuwa akipigania haki ya mwanawe katika mahakama ya Iraq. Aliuwawa kwa kupigwa risasi Machi 2020.

Baadhi ya mauwaji, kama ya al-Hashimi, al-Wazni na Aboud baba yaliweza kunaswa kupitia kamera za usalama.  Na vidio zimeonesha kwa kiwango fulani cha kufanana kwa namna gani wauwaji walivyokuwa wakiwasili katika maeneo ya tukio, wakiwa na gari au pikipiki.  Wengi waliouwawa ni wakosoaji kwa kuhusishwa tu na hujuma ya kikosi maalumu cha ulinzi nchini Iraq kinachojulikana kama PMF.

Soma pia:Kituo cha jeshi la Marekani chashambuliwa Iraq 

Kikosi hicho PMF, ambacho kiliundwa mahususi kwa ajili ya kukabiliana na kundi la Dola la Kiislamu  ambapo pamoja na adui yao mkubwa kuangamizwa kwa kiasi kikubwa, idadi kubwa ya wapiganaji wa PMF bado wanaendeleza utiifu kwa Iran. Iran ndiyo iliyokuwa ikitoa msaada wa vifaa, mafunzo ya kijeshi na fedha wakati wa makabiliano yake na kundi la Dola la Kiislamu.

PMF yashukiwa kuhusika na mauaji

Inaaminika kwamba utekaji nyara na mauwaji vinafanywa na PMF au kikundi kipya cha kuteleza harakati hizo. Wanaharakati wamekuwa wakizitoa tuhuma hizo waziwazi kabisa, jambo ambalo wanasema limekuwa likisababishwa waishi katika vitisho kila siku.

Irak Bagdad Trauerprozession für Wissam Alyawi der Asaib Ahl Al-Haq-Fraktion
Wanachama wa kundi la Hashed al-Shaabi, au PMF ambao wanadaiwa kuhusika na mauaji ya wanaharakati na wakosoaji wa utawala na uingiliaji wa Iran.Picha: AHMAD AL-RUBAYE/AFP/Getty Images

Wawili miongoni mwao wameliambia shirika la habari la DW, kwamba wengi miongoni mwao wanaishi kwa kificho. Mmoja miongoni mwa hao amenukuliwa akisema "Kuna kampeni ya nguvu ya kutaka niuwawae, na najua nipo hatarini" Bwana huyo alizungumza kwa masharti ya kutolitaja jina lake.

Kwa pamoja walisema wamezifunga kurasa zao za mitandao ya kijamii na kubadili akauti zao za barua pepe pamoja na nambari za simu. Wanasema baadhi yao wanabadili maeneo ya kulala kila usiku, kuhama kutoka nyumba moja kwenda nyingine. Huku wengine wanajaribu kuondoka katika nchini humo.

Iraq kwatibuka tena

Wanahakati wameiambia DW kwamba wana imani kuwa maelfu ya watu miongoni mwao wamekimbia nchini Iraq kutokana na uwepo wa kampeni ya kuwatesa na kuwauwa. Matukio hayo hayawalengi waandamanaji tu, lakini pia waandishi wa habari, na majaji.

Chanzo: DW