1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Ethiopia na ONLF watiliana saini makubaliano

Caro Robi
22 Oktoba 2018

Kundi la Waasi la Ogaden National Liberation Front ONLF na serikali ya Ethiopia wametiliana saini mkataba wa amani.

https://p.dw.com/p/36wb0
Mitglieder der ONLF/Ogaden National Liberation Front
Picha: Getty Images/A.Maasho

Serikali ya Ethiopia imetiliana saini makubaliano ya amani na kundi la waasi la Ogaden National Liberation Front ONLF linalotokea jimbo la Somali.

Kundi hilo awali lilikuwa limepigwa marufuku na kuorodheshwa kama kundi la kigaidi. ONLF ilianzisha azma ya kutaka jimbo la Somali ambalo pia linajulikana Ogade kujitenga na kujitawala mnamo mwaka 1984.

Mwaka 2007, jeshi la Ethiopia lilianzisha operesheni kubwa dhidi ya kundi hilo baada ya waasi hao kuwaua watu 74 katika shambulizi lililolenga kiwanda cha mafuta kinachoendeshwa na Wachina.

Mapema mwaka huu, bunge lililiondoa kundi hilo la ONLF kutoka orodha ya makundi yaliyopigwa marufuku kama sehemu ya kuunga mkono mageuzi ya Waziri mkuu Abiy Ahmed ambaye amejaribu kufikia maridhiano na wapinzani wa serikali.

Mnamo mwezi Agosti, ONLF lilitangaza limesitisha mapigano. Makubaliano ya amani yaliyofikiwa jana inazitaka pande zote mbili  kukomesha uhasama na inaendeleza harakati  zake za kisiasa kwa njia ya amani.