Sera ya wakimbizi ya Merkel yashambuliwa tena | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.07.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Sera ya wakimbizi ya Merkel yashambuliwa tena

Mshirika muhimu wa Kansela Angela Merkel wa Ujerumani Jumamosi (30.07.2016) kwa mara nyengine tena amejitenganisha na sera yake ya kuwakaribisha wahamiaji nchini kufuatia mfululizo wa mashambulizi ya kikatili nchini

Horst Seehover waziri mkuu mhafidhina wa jimbo la Bavaria amesema hakubaliani na kauli mbiu ya Merkel kwamba "tunaweza " ya kuwapatia hifadhi takriban wahamiaji na wakimbizi milioni moja na laki moja walioingia nchini mwaka 2015.

Seehofer ambaye anakiongoza chama cha Christian Demokrat (CSU) ambacho ni chama ndugu kwa chama cha kihafidhina cha Merkel cha Christian Demokrat (CDU) amesema kwa nia njema yote hawezi kuitumia kauli hiyo kama yake.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano na serikali ya jimbo la Bavaria huko Tegernsee amesema hadi sasa hatua za kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo aliloiita kuwa kubwa mno zimekuwa hazikidhi haja.

Akisisitiza kwamba hana nia ya kuanzisha ugomvi na chama cha Merkel amesema ni muhimu kukabili uhalisia kinagaubaga.

Mashambulizi yasababisha maafa

Kansela Angela Merkel na Waziri Mkuu wa jimbo la Bavaria Horst Seehofer.

Kansela Angela Merkel na Waziri Mkuu wa jimbo la Bavaria Horst Seehofer.

Mashambulizi matano yaliyotokea Ujerumani tokea Julai 15 yamesababisha watu 15 kupoteza maisha yao wakiwemo washambuliaji wanne na watu wengine kadhaa kujeruhiwa. Washambuliaji wawili kati yao walikuwa na uhusiano na kundi la Dola la Kiislamu.

Kauli ya Seehofar ambaye jimbo lake ndio lililoathirika zaidi katika mashambulizi hayo inakuja baada ya Merkel hapo Alhamisi kutetea kauli yake mbiu ya "tunaweza" na kuahidi kutoyumba kutoka sera yake ya kuwakaribisha wakimbizi.

Merkel amesema hatowaruhusu wapiganaji wa jihadi kuizuwiya serikali yake iongozwe na hoja na huruma.

Amesema licha ya matukio hayo kuzusha mashaka makubwa hofu haiwezi kuongoza maamuzi ya kisiasa.

Merkel alitangaza mpango wa vipengele tisa kukabiliana na mashambulizi ya kigaidi ikiwa ni pamoja na hatua za kuajiri wafanyakazi zaidi wa mashirika ya usalama na kuwepo na mfumo wa kutowa tahadhari na mapema kuhusiana na kupandikizwa itikadi kali kwa wakimbizi.

Umashuhuri wa Merkel

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.

Umashuhuri wa kansela ulikuwa umeshuka kutokana na mzozo wa wakimbizi na yumkini ukapata pigo tena baada ya kuongezeka kwa muda kufuatia Uingereza kupiga kura kujitowa Umoja wa Ulaya mwezi uliopita.

Merkel anakabiliwa na shutuma kwenye mtandao wa kijamii baada ya kushindwa kutamka kitu hadi siku ya pili ikiwa ni masaa 17 baada ya Rais Barack Obama wa Marekani kulaani mashambulizi yaliyotokea Munich nchini Ujerumani ambapo Mjerumani mwenye asili ya Iran kuwaua kwa kuwapiga risasi watu tisa.

Kauli ya Seehofer inazidi kufanya iwe ngumu kwa Merkel kuendelea kutetea sera yake ambayo inakosolewa kwa kusababisha mashambulizi hayo jambo linalohatarisha pia umashuhuri wake kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu hapo mwakani.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP

Mhariri :Sylvia Mwehozi

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com