1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sera ya maendeleo ya Ujerumani kwa bara la Afrika yakosolewa

Zainab Aziz Mhariri: Daniel Gakuba
5 Aprili 2019

Mashirika ya misaada kwenye ripoti yake mpya inayoitwa "Compass 2019", yamesema vipaumbele vingi sio sahihi. Mashirika hayo yamesema serikali ya Kansela Angela Merkel haizingatii nchi za Afrika zinazohitaji misaada.

https://p.dw.com/p/3GIa4
Uganda Bundesentwicklungsminister Gerd Mueller CSU bei der Besichtigung der Firma Ibero Uganda Ltd
Picha: Imago/Photothek

Wiki iliyopita, Serikali ya Ujerumani iliamua kufanya marekebisho kwenye sera yake juu ya Afrika, ambapo sasa mpango huo unatilia maanani umuhimu mkubwa wa bara hilo. Baadaye mwaka huu, mfuko mpya wa dola bilioni moja utazinduliwa, kwa ajili ya kuyasaidia makampuni ya Ujerumani pamoja na yale ya Afrika yatakayowekeza katika barani Afrika.

Baraza la Mawaziri pia limerefusha muda wa kuhudumu wanajeshi wa Ujerumani huko nchini Mali, licha ya kuendelea kuzorota hali ya usalama nchini humo. Hata hivyo mashirika mawili ya msaada ya Welthungerhilfe na "Terre des Hommes" yameikosoa sera hiyo.

Katika ripoti mpya ya mashirika hayo - "Compass 2019: kuhusu sera ya Maendeleo ya Ujerumani, yameonya kuwa mipango hiyo Ujerumani kwa bara la Afrika inakabiliwa na ukosefu wa fedha. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hakuna hata nchi moja ya Afrika iliyo kwenye orodha ya wapokeaji 10 wakubwa wa misaada ya maendeleo ya Ujerumani.

Katibu mkuu wa shirika la misaada la Welthungerhilfe Mathias Mogge amesema vipaumbele vinavyopasa kupewa umuhimu havipewi umuhimu huo na mara nyingi masuala ya uhamiaji ndio yanapewa kipaumbele zaidi.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa/M. Schutt

Katibu mkuu wa shirika la misaada la Welthungerhilfe Mathias Mogge amesema nchi nyingi maskini zitaachwa pembeni. Kulingana na ripoti ya  "Compass 2019", nchi 33 maskini zaidi duniani zipo barani Afrika. Nyingi kati ya nchi hizo hazivutii uwekezaji wa kibinafsi, kwa sababu zinakabiliwa na migogoro, vita na pia utawala mbaya.

Kwa mtazamo wa mashirika hayo ya misaada, uratibu wa sera ya Ujerumani juu ya Afrika lazima uimarishwe. Baada ya Ujerumani kushikilia wadhfa wa urais wa kundi la nchi 20 zenye utajiri wa viwanda (G20) mnamo mwaka 2017, wizara mbalimbali zilianzisha mipango kuhusu bara la Afrika.

Wakosoaji wamelalamika kwamba wakati mwingine hatua hizo zinapishana katika kulitimiza lengo kuu. Wakati mpango wa wizara ya Maendeleo ya Ujerumani maarufu kama  "Marshall Plan for Afrika" unasisitiza umuhimu wa demokrasia na haki za binadamu, Wizara ya Fedha inafanya kazi na nchi kama Rwanda na Togo zenye watawala wanaotumia nguvu dhidi ya raia wake kwenye mpango wake wa "Compact with Africa."

Kwa mujibu wa serikali ya Ujerumani, mwongozo mpya unapaswa kuhakikisha kuwa mipango hii mbalimbali inazingatia lengo moja linalofanana. Hata hivyo, haijulikani bado jinsi mipango hiyo itakavyofanya kazi pamoja.

Mashirika ya misaada ya Ujerumani yanaunga mkono ajenda ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2063. Mpango huo wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii wa bara hilo uliundwa na wakuu wa serikali za Afrika. Katika mwongozo wake mpya katika sera ya Afrika, serikali ya Ujerumani inasisitiza kuwa inataka kufuata maelekezo hayo. Hata hivyo, mashirika ya Welthungerhilfe na Terre des Hommes yanataka hatua zaidi za vitendo zichukuliwe, kama vile mipango ya pamoja kati ya Ujerumani na Umoja wa Afrika. Wakuu wa mashirika hayo ya misaada wamesema Ujerumani inapaswa kuzingatia upya vipaumbele vyake  kimataifa. 

Chanzo: LINK: http://www.dw.com/a-48201834