1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
HistoriaAfrika

Sengbe Pieh: Shujaa wa meli ya Amistad

Yusra Buwayhid
10 Oktoba 2020

Sengbe Pieh, kutoka Sierra Leone alikamtwa na kutumbukizwa kwenye utumwa 1839. Wakati akisafirishwa na wenzake kwenye meli ya Amistad kuelekea Cuba, Pieh aliongoza uasi dhidi ya waliowakamata.

https://p.dw.com/p/3dui1
African Roots | Sengbe Pieh 1 | Porträt

Sengbe Pieh: Mtumwa aliyepambana kurudi nyumbani

Sengbe Pieh alizaliwa wapi? Siku halisi aliyozaliwa Sengbe Pieh haijulikani, lakini wanahistoria wengi wanakisia alizaliwa mnamo mwaka 1814 katika eneo linalojulikana leo hii kama Sierra Leone. Inaaminika kwamba alizaliwa katika kisiwa cha kusini mwa wilaya ya Bonthe, ambacho ni maarufu kwa uvuvi na kilimo. Pieh aliwa mkulima wa mpunga. Na wakati wa kukamatwa kwake, inasemekana Pieh alikuwa na mke, watoto wawili wa kike na mmoja wa kiume.

Sengbe Pieh anatoka kwenye kabila gani? Ingawa wengi wanaamini anatoka katika kabila la Mende, moja ya makabila makubwa Sierra Leone, baadhi ya wanahistoria wanadai kwamba alikuwa ni kutoka kabila la Shebro. Kisiwa cha Bonthe ambacho pia kinajulikana kama Kisiwa Shebro, kilikaliwa kwa mara ya kazwa na watu wa kabila la Shebro, moja ya makabila madogo nchini Sierra Leone. Watu wa kabila la Mendes inasemekana walihamia baadae katika kisiwa hicho. Kutokana na ndoa za kuingiliana baina ya makabila, watu wengi wa kabila la Shebros hivi sasa wanajiona kama Mende. Watu wa makabila hayo mawili wameingiliana sana, kiasi ya kwamba ni vigumu kutofautisha kati ya Shebro na Mende nchini Sierra Leone.

African Roots | Sengbe Pieh 5
Meli ya Amistad

Je, uasi katika meli ya Amistad ulitokana na kitu gani? Mnamo Januari 1839, akiwa analima kwenye shamba lake la mpunga, Senghe Pieh alitekwa nyara na kuuzwa kwa wafanyabiashara ya utumwa kutoka Uhispania katika mji wa Sulima, Kusini mwa Sierra Leone. Pieh na wenzake wengi kutoka Sierra Leone walisafirishwa kwa nguvu hadi Havana huko Cuba ambako waliuzwa mnadani.

Wakati yeye na wenzake wakiwa kwenye meli ya 'La Amistda' wakipelekwa kwenye mashamba ya miwa kwenda kutumikishwa kama watumwa, Pieh aliweza kujifunguwa minyororo aliyokuwa amefungwa. Na baada ya Pieh kuwafunguwa wenzake kadhaa, waliwavamia waliokuwa wamewakamata kwa kutumia visu vya kukatia miwa.

Walimuua nahodha wa meli hiyo ya kusafirishia watumwa pamoja na mpishi, na Pieh kuamrisha warejeshwe Afrika. Kutokana na kwamba hawakuwa na uzoefu wa ubaharia, nahodha mpya aliyechukuwa udhibiti wa meli hiyo aliwadanganya Waafrika hao waliokuwa wakiongozwa na Pieh, na usiku ulipoingia  aliigeuza meli kuelekea Cuba. Bila ya kutarajia, ulipiga upepo mkali na kuisogeza meli hiyo kwenye mwambao wa Marekani. Pieh na wenzake walikamatwa na kushtakiwa kwa madai ya mauaji na uharamia katika mahakama ya Marekani.

African Roots | Sengbe Pieh 4
Asili ya Africa | Sengbe Pieh

Lakini kundi la wanaharakazi wa kukomesha utumwa ambalo baade lilikuja kujulikana kama "Kamati ya Amistad” liliweza kutoa hoja nzito wakiwatetea Waafrika hao kuwa waliokamatwa na kuuzwa kama watumwa kinyume na sheria, na hatimaye kushinda kesi hiyo. Ingawa waliachiliwa huru na kuruhusiwa kurudi nyumbani, wengi miongoni mwao walipoteza maisha wakiwa safarini, na hasa katika mapigano ya uasi yaliyoongozwa na Sengbe Pieh. Baada ya kamati ya Amistad kufanikiwa kukusanya pesa za kutosha, Pieh na wenzake waliobakia walirudi Sierra Lione wakifuatana na baadhi ya wamishionari wa Kimarekani mnamo Januari 1842.

Kuna uhusiano gani kati ya mkasa huu na kukomeshwa kwa utumwa nchini Marekani? Tukio hili kwa kiasi kikubwa lilichangia kuibuka kwa vuguvugu la kukomesha utumwa, ambalo lilifanya kampeni ya kumaliza utumwa nchini Marekani. Hakuna kitabu kinachozungumzia historia ya utumwa nchini Marekani, bila ya kutaja mkasa huu wa ushujaa wa Sengbe Pieh. Hadithi ya Sengbe Pieh inafundishwa katika baadhi ya vyuo vikuu nchini Marekani, na katika baadhi ya majimbo nchini humo yana masanamu ya Sengbe Pieh. Hollywood imetengeneza filamu juu ya hadithi hiyo ya Sengbe Pieh. Kurejea kwa Sengbe Pieh nchini Sierra Leone pia kulifungua milango kwa wamishionari kusambaza dini ya Kikristo nchini humo.

Sengbe Pieh: Mtumwa aliyepambana kurudi nyumbani

Sengbe Pieh alizikwa wapi baada ya kufariki kwake? Sengbe Pieh alifariki mnamo mwaka 1879. Haijulikani hakika kama aliweza kukutana tena na familia yake. Inaaminika Sengbe Pieh alizikwa Bonthe, Sierra Lione. Sengbe Pieh alikuwa mwanachama wa jamii ya Poro, ambayo ni jamii ya jadi ya kisiri. Kwa namna hiyo, kaburi lake linajulikana tu na wanajamii wenzake wa Poro. Wizara ya Utalii imepanga kuyafukuwa mabaki ya Sengbe Pieh, na kuyazika katika eneo lingine ambako kaburi lake linaweza kutembelewa na umma.

Sengbe Pieh anakumbukwa kwa yepi mengine? Sengbe Pieh aliamini kuwa binadamu wote ni sawa, bila kujali rangi au kabila. Alipigania uhuru wake na uhuru wa wengine.

Sierra Leoneans inamkumbuka vipi? Picha yake inapatikana kwenye noti ya Sierra Leone. Daraja moja katika mji mkuu wa Freetown hivi karibuni lilipewa jina lake. Ni rahisi kuona picha zake zilizochorwa kwenye mitaa ya Freetown.

Ushauri wa kisayansi kuhusu makala hii umetolewa na wanahistoria Profesa Doulaye Konaté, Lily Mafela, Ph.D., na Profesa Christopher Ogbogbo. Mfululizo wa makala za Asili ya Afrika umefadhiliwa na Taasisi ya Gerda Henkel.